KIGOMA, Septemba 4, 2026 — Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma imemhukumu Nicholaus Komba Mahitana maarufu kama Abdallah Mahimbo baada ya kukiri makosa ya kughushi, kujifanya mtumishi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na kuwalaghai wanufaika wa mikopo kwa madai kuwa angeweza kuwafutia madeni yao.
Mahakama imemuamuru Mahitana kulipa faini ya Shilingi milioni 1.6 na kurejesha Shilingi milioni 3, pamoja na kuripoti katika Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Mbeya mara moja kila mwezi kwa kipindi cha miaka mitatu.
Kesi hiyo imehitimishwa leo, Ijumaa, baada ya mtuhumiwa kumuandikia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) akiomba kuingia katika makubaliano ya kukiri kosa (Plea Bargaining).
Hukumu hiyo imeshuhudiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, ambaye amewataka wanufaika wa mikopo kufuata taratibu rasmi za urejeshaji wa mikopo na kuepuka kutumia vishoka wanaodai kuwa na uwezo wa kufuta madeni.
Dkt. Kiwia ameonya kuwa vitendo vya kutumia njia zisizo rasmi vinaweza kuwaingiza wanufaika katika matatizo makubwa, ikiwemo kupoteza fedha na kuhatarisha ajira zao.
HESLB imeendelea kusisitiza kuwa wanufaika wanapaswa kutumia njia na taratibu rasmi katika masuala yote yanayohusu urejeshaji wa mikopo na kuepuka watu wanaojitambulisha kama mawakala wenye uwezo wa kufuta madeni.





No comments:
Post a Comment