SERIKALI YAITAKA BODI YA WATAALAAM WA MIPANGOMIJI KUWEKA MATUMIZI BORA YA ARDHI

Na Jonas Kamaleki, MAELEZO 

SERIKALI imeitaka Bodi ya Usajili wa Wataalaam wa Mipangomiji kuweka mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa maendeleo ya wanachi na Taifa kwa ujumla.

Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Yamungu Kayandabila katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano wa Tatu wa Bodi ya Usajili wa Wataalaam wa Mipangomiji.

“Ardhi ni msingi wa kipekee wa maendeleo na ni raslimali isiyoongezeka kwa sababu hiyo mipango bora ya matumizi ya ardhi sio hiari bali ni lazima kwa Taifa lolote Ulimwenguni,”alisema Kayandabila.

Akisisitiza umuhimu wa ardhi, Kayandabila ametumia maneno ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyewahi kusema kuwa ili tuendelee tunahitaji Ardhi, Watu, Siasa Safi na Uongozi Bora

Katibu Mkuu huyo amekemea vitendo vya baadhi ya watumishi wa serikali kutozingatia maadili ya kazi zao katika suala la mipangomiji ikiwemo rushwa. Amesema Serikali itachukua hatua kali na za haraka dhidi ya watumishi hao.

Kayandabila amebainisha kuwa matatizo mengi yanayojitokeza mijini yanasababishwa na kutokuwa mipango mizuri ya matumizi ya ardhi mfano majitaka kutokuwa na namna nzuri ya kuyashughulikia imesababisha matatizo ya kipindupindu. Hivyo lazima kuwepo na mipango kamambe (Master Plan) ya miji na majiji.

Amesisitiza mipangomiji ianinishe maeneo mbali mbali kwa ajili ya makazi, shule, maeneo ya wazi, viwanda, hospitali, barabara na huduma nyingine za jamii. 

Ameitaka Bodi kuhakikisha inaeleweka kwa wananchi ili iweze kuwahudumia kama zilivyo bodi nyingine kama vile Bodi za Wahasibu (NBAA), Wakandarasi (CRB), Wahandisi (ERB) na Bodi ya Wafamasia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wataalaam wa Mipangomiji, Prof. Wilbard Kombe amesema Bodi hii imeundwa ili kusimamia taaluma na kuboresha ufanisi katika mikakati ya maendeleo ya nchi na ni chombo muhimu cha kudhibiti vitendo vya utovu wa nidhamu miongoni mwa wahusika na kuziba mianya ya fani kuingiliwa kiutendaji na watu wasio na taaluma hiyo.

Prof. Kombe ameongeza kuwa Bodi inakuza ujuzi na weledi wa kitaaluma kwa lengo la kuboresha na kuongeza mchango wake kwenye kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa Taifa kwa ujumla.
Kauli Mbiu ya Mkutano huo ambao umeanza leo ni “Upangaji Miji: Kwa uhakika wa milki za uzalishaji”

Comments

Popular posts from this blog

JESHI LA MAGEREZA NCHINI WAJADILIANA NA NHC NAMNA YA KUENDELEZA MAKAZI MAKAO MAKUU DODOMA

Baraza Jipya la Mawaziri