MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA AKEMEA TAMKO LA CHADEMA

indexNimepokea kwa masikitiko tamko la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) lililotolewa jana tarehe 27 Julai, 2016 kupitia vyombo vya habari, kuhusu hali ya demokrasia ya vyama vingi hapa nchini. Tamko hilo limejaa lugha ya uchochezi, kashfa, kuudhi na lenye kuhamasisha uvunjifu wa amani. Ili kuepuka kurejea tamko lote, nimeona ni vyema nitoe mfano wa maneno yafuatayo yaliyosemwa, ambayo yanakiuka Sheria ya Vyama vya Siasa:-
“CHADEMA tunasema tunaitangaza siku ya tarehe 1 Septemba, 2016 kama siku ambayo itakuwa ni siku ya mikutano nchi nzima ikiwamo maandamano ambapo ngazi zetu mbalimbali za chama kuanzia ngazi ya msingi hadi Taifa tutafanya mikutano in defiance ya order ya Rais, ya Jeshi la Polisi kwamba haturuhusiwi kufanya mikutano ya kisheria”
Kimsingi, Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka 1992 kifungu 9 (2)(c) inakataza chama cha siasa kutumia au kuhamasisha matumizi ya nguvu au vurugu kama njia ya kufikia malengo yake ya kisiasa.
Aidha, kifungu cha 9(2)(f) kinakataza chama cha siasa kuruhusu viongozi au wanachama wake kutumia lugha ya matusi, kashfa na uchochezi ambayo inaweza kusababisha au ikapelekea kutokea uvunjifu wa amani. Vile vile kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa, Tangazo la Serikali namba 215 la mwaka 2017, zinakataza chama cha siasa kutumia lugha za matusi, kashfa, uongo na uchochezi.
Kanuni ya 5(1)(d) inakitaka kila chama cha siasa kutotoa maneno yoyote au maandishi ambayo ni uongo. Kuhusu mtu yoyote au chama cha siasa chochote.
Kanuni ya 5(1)(f) inasema kuwa, kila chama cha siasa kina wajibu wa kulaani na kupinga yafuatayo:-
(i)                  Matumizi ya lugha ya matusi;
(ii)                 Vitendo vya kibabe na vurugu; na
(iii)   Matumizi ya nguvu ili kujipatia umaarufu wa chama au sababu yoyote ile.
Hivyo, tamko la CHADEMA ni ukiukwaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa. Aidha, hii siyo mara ya kwanza kwa CHADEMA kutumia lugha za namna hii za kuhamasisha uvunjifu wa amani (civil disorder).
Natumia fursa hii kukemea tamko hilo hadharani, kwa mujibu wa kanuni ya 6(2) ya Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa. Pia nawaasa CHADEMA wasiendeleze tabia hii.
Mwisho, napenda kusisitiza kuwa, kwa dhamana niliyopewa kama Msimamizi wa Sheria ya Vyama vya Siasa, napenda kutumia fursa hii kuviasa vyama vyote vya siasa vitimize wajibu wao kwa weledi kama taasisi za kisiasa.
Ni vema Viongozi wa Vyama vya Siasa  wakaonyesha taswira stahiki ya wanasiasa wakomavu, au Vyama vya Siasa vya kutolea mfano ndani na nje ya mipaka yetu, kwa kuzingatia Sheria za Nchi katika kuendesha shughuli za kisiasa.
Vyama vya Siasa viepuke vitendo, kauli au matamshi yenye mlengo wa kusababisha uchochezi au kufarakanisha Umma na Serikali yao.
Madhali zipo Sheria na njia stahiki za kidemokrasia za mawasiliano na Taasisi za Umma, basi navisihi Vyama vyote vya Siasa kuzingatia utaratibu huo wa mawasiliano kwa mujibu wa Sheria zilizopo. Aidha, uvumilivu wa kisiasa katika azma za kudumisha ukuaji wa kidemokrasia nchini haukwepeki.
Tudumishe amani ya nchi yetu.
“MUNGU IBARIKI TANZANIA”
Jaji Francis S.K. Mutungi
MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA

28 Julai, 2016

Comments

Popular posts from this blog

JESHI LA MAGEREZA NCHINI WAJADILIANA NA NHC NAMNA YA KUENDELEZA MAKAZI MAKAO MAKUU DODOMA

Baraza Jipya la Mawaziri