MAJALIWA AKAGUA MADARASA YA SEKONDARI YA LINDI YALIYOUNGUA MOTO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua maabara na madarasa yaliyoungua kwa moto katika shule ya sekondari ya Lindi akiwa katika ziara ya mkoa huo Julai 14, 2016  Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

NDI2

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaahidi Walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Lindi kwamba Serikali itahakikisha miundombinu  iliyoungua moto inakarabatiwa kwa haraka ili shughuli za masomo ziweze kuendelea kama awali.
Pia amewataka wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi siku ya Jumapili (Julai 17, 2016) katika harambee ya kuchangia ukarabati wa miundombinu ya shule hiyo.
Waziri Mkuu alitoa ahadi hiyo leo (Alhamisi Julai 14,2016) wakati alipotembelea shule hiyo kwa ajili ya kujionea athari zilizosababishwa na moto uliotokea usiku wa kuamkia Julai 10 mwaka huu na kuunguza vyumba tisa vya madarasa.
 “Mkoa tayari umeshafanya tathimini ya athari zilizobabishwa na moto huo hivyo naomba tuletewe taarifa ya tathmini hiyo ya uharibifu wote pamoja na gharama zinazohitajika ili tuhakikishe miundombiunu hii inarudi na shughuli ziweze kuendelea kama awali,” amesema.
“Nawaomba walimu na watumishi wengine shuleni hapa kuendelea kufanya kazi katika mazingira haya na kwamba Serikali itarudisha miundombinu iliyoharibika kwa haraka,” alisema.
Akisoma taarifa ya ajali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi alisema chanzo cha moto huo ni kutokea kwa tatizo la umeme kwenye chumba cha ofisi ya walimu.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema maafa hayo yameathiri shule hiyo kwa asilimia 34 na kusababisha hasara ya sh. milioni 682.78.
“Moto huu umetokea siku moja kabla ya kufunguliwa kwa shule.Uongozi wa Mkoa unaendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha shule hiyo inarudi katika hali yake ya kawaida,” alisema.
Zambi alitaja miundombinu mingine iliyoathirika na moto huo kuwa ni jengo lenye matundu 26 ya vyoo na jengo la maabara ya kemia na fizikia ambalo litahitaji upauaji upya baada ya paa lake kuteketea kwa moto.
Alisema kwa sasa masomo yanaendelea kama kawaida shuleni hapo ambapo wanafunzi wanasomea katika bwalo la chakula pamoja na kwenye chumba cha maabara cha baiolojia.

Comments

Popular posts from this blog

JESHI LA MAGEREZA NCHINI WAJADILIANA NA NHC NAMNA YA KUENDELEZA MAKAZI MAKAO MAKUU DODOMA

Baraza Jipya la Mawaziri