Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Bw. Nicholous Kombe
akimsikiliza Meneja wa Huduma kwa Jamii wa NHC Bw. Muungano Saguya akimshukuru
kwa Halmashauri hiyo kusaidia kikundi cha vijana kwa kuwawezesha fedha na
udongo kwa ajili ya kutengeneza matofaliya kufungamana. Katikati ni Meneja wa
NHC Mkoa wa Lindi Bw. Mussa Patrick Kamendu.
Kikundi cha vijana cha Ruangwa Materials Group katika Halmashauri ya Wilaya
Ruangwa kimeshatengeneza matrofali kwa kutumia mashine ya msaada kutoka NHC.
Halmashauri ya Wilaya hiyo imeamua kuyatumia matofali ya vijana hawa kujengea
zahanati na majengo mengine yanayohitajika katika Halmashauri zikiwemo nyumba
za Waalimu.
Jengo la Ofisi ya kikundi cha vijana cha Narunye(hakuna kutegeana) katika
Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Vijijini likiwa limeonwa na Kiongozi wa mbio za
mwenge wa Uhuru kama inavyoonekana. Kikundi hiki kimeshaanza kupata maombi mengi
ya matofali kutoka kwa wananchi wanaohitaji.
Meneja wa NHC Mkoa wa Lindi Bw. Mussa Patrick Kamendu akitoa mawaidha
kwa kikundi cha vijana cha Narunye
kilichopo katika Wilaya ya Lindi vijijini baada ya kutembelea kikundi
hicho kukagua kazi zake.Vijana hawa wanajihusisha pia na utunzaji mazingira.
Baada ya Wakurugezi wa Halmashauri za Kilwa na Lindi Vijijini kutokuwa
karibu na vikundi vya vijana, Meneja wa Huduma kwa Jamii wa NHC na Meneja wa Mkoa
wa Lindi waliweza kufanya mazungumzo nao ya kina na hatimaye wamekubali kuwasaidia
vijana waliopewa msaada wa mashine na NHC katika Halmashauri zao ili waweze
kujiajiri. Kulia ni Bi. Oliver Vavunge ambaye
ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Vijijini na wa pili
kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Kilwa Bi. Maimuna Mtanda.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Bw. Daniel Kaluse hakuwa nyuma kutembelea kikundi
cha Vijana na Maendeleo kilichopo eneo la Mitwero nje kidogo ya Manispaa hiyo ili
kuwapa moyo na kufahamu maendeleo yao akiwa ameandamana na ujumbe wa NHC.
Meneja wa NHC Mkoa wa Mtwara Bw. Joseph John akitoa taarifa ya Mkoa kwa
Meneja wa Huduma kwa Jamii wa NHC ya maendeleo ya vikundi vya vijana
waliosaidiwa mashine na NHC . Katika taarifa yake Meneja huyo alisikitishwa na
vijana wa Mkoa wa Mtwara kushindwa kutumia kikamilifu msaada huo na akalaumu
Halmashauri za Mkoa huo kushindwa kushiriki kikamilifu katika programu hiyo ya
kusaidia vijana.
Meneja wa Huduma kwa Jamii wa NHC Bw. Muungano Saguya akikemea na
hatimaye kukinyanganya mashine kikundi cha Likonde katika Manispaa ya Mtwara
kwa kuifungia stoo mashine waliyopewa msaada na NHC bila kufanya kazi iliyokusudiwa ya kufyatua
matofali. Mashine hiyo itapewa kikundi kingine ili itumike kikamilifu.
Meneja wa Huduma kwa Jamii wa NHC Bw. Muungano Saguya akiwa Wilayani
Tandahimba akikagua matofali yaliyotengenezwa na kikundi cha vijana cha
Maendeleo Group kilichopewa msaada wa mashine
na NHC. Kikundi hiki kinasubiri kulipwa na Halmashauri matofali hayo
yanayotarajiwa kujengea nyumba za waalimu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tandahimba Bw Dennis Mwaitete akielezea
mkakati wa Halmashauri yake wa kusaidia vijana ulivyo alipotembelewa na ujumbe
wa NHC uliokuwa ukihakiki vikundi vya vijana Mkoani Mtwara.
Kikundi cha vijana cha Umoja
Lekanelo kilichopo Wilaya ya Newala
kilichoshindwa kutumia kikamilifu mashine ya msaada kilichopewa na NHC
kiliweza kupokonywa mashine hiyo jana. Wilaya ya Newala ina shughuli za madini
na kilimo cha korosho kiasi cha kuwafanya vijana kushindwa kujihusisha
kikamilifu na mradi wa kufyatua matofali.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Marx Kamaoni akizungumza na ujumbe wa NHC
uliofika Ofisini kwake kuhamasisha Halmashauri za Wilaya kusaidia vikundi vya
vijana vilivyopewa msaada wa mashine za kufyatulia matofali na NHC.
Vyombo vya habari vimehusishwa katika uhakiki huu na hapa Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Newala Bw. Marx Kamaoni akiongea na waandishi wa
habari kuelezea mkakati wa Halmashauri yake kusaidia vijana.
Kikundi cha Vijana cha For Energy Group kilichopo Wilayani Masasi
kilitembelewa na baada ya kuridhishwa na
utendaji wake NHC ilikiongezea mashine mbili zilizopokonywa vikundi vingine
vilivyoshindwa kuzitumia Wilayani Newala na Masasi Vijijini. Hii ni nyumba
iliyojengwa na kikundi hicho Wilayani Masasi.
Meneja wa Huduma kwa Jamii wa NHC Bw. Muungano Saguya akivionya vikundi vya vijana vya Nayoden na Mangaka Wilayani Nanyumbu
waliokula fedha ya mtaji waliopewa na NHC ambapo aliamuru kuchukuliwa kwa
mashine zao na kuwapa muda wa kujiandaa. Aliwataka kuziomba mashine hizo kwa
maandishi watakapokuwa tayari kuzitumia. Mashine hizo zilifungiwa Ofisi ya Kata
ya Mangaka kwa muda wa miezi nane wakisubiri kupata fedha nyingine kutoka NHC.
Mashine iliyopokonywa vijana wazembe Wilayani Nanyumbu ikipandishwa
katika gari baada ya vijana hao kuzembea kuitumia na kuifungia Ofisi kwa muda
mrefu.
Uhakiki wa vikundi vya vijana vilivyopewa msaada wa mashine na NHC ili kujiajiri na kusaidia wananchi kupata matofali ya kujengea nyumba bora umeanza katika Mikoa mbalimbali ukianzia na Mkoa wa Lindi na Mtwara. Katika hali isiyotarajiwa Mkoa wa Mtwara ambao kwa muda mrefu umekuwa ukililia kuletewa maendeleo umeshindwa kutumia fursa ya msaada wa mashine kwa vijana waliyopewa na NHC hali iliyolifanya Shirika kutwaa baadhi ya mashine ili zipewe vikundi vingine vinavyofanya vizuri Fuatilia kupitia habari picha hizi ili ufahamu kilichojiri katika mikoa hiyo ya kusini mwa Tanzania. Leo uhakiki huo unaendelea Mkoani Ruvuma.
No comments:
Post a Comment