Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum, Haji Omar Kheir alienyoosha mikono akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mradi wa Uwekaji Kamera za kiusalama katika mji wa Zanzibar Ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar.
Mwandishi wa Habari Mwandamizi wa ITV, Farouk Karim wakwanza ( kushoto) ,akiuliza maswali katika mkutano wa Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum Haji Omar Kheir na Waandishi wa Habari akielezea mradi wa Uwekaji Kamera za kiusalama katika mji wa Zanzibar Ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar.
……………………………………………………………….
Na Ramadhani Ali Maelezo ZANZIBAR
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha mradi mkubwa wa kiulinzi katika maeneo mbali mbali ya Mji wa Zanzibar katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu vinavyoendelea kuongezeka kila siku.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara maalum Haji Omar Kheir ameeleza hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema katika siku za karibuni Zanzibar imeshuhudia vitendo vya uhalifu ikiwemo ujambazi, uporaji, hujuma, kuwamwagia watu tindikali pamoja na matokeo ya uchomaji moto mali za umma, taasisi na watu binafsi.
Hali hiyo imeleta wasi wasi mkubwa kwa wananchi na wageni wanaoitembelea Zanzibar kitu ambacho kinaweza kuathiri biashara ya Utalii inayoingiza fedha nyingi za kigeni.
Alieleza kuwa mradi huo utahusisha uwekaji wa Kamera za kiulinzi katika maeneo yote ya Mji Mkongwe na baadhi ya maeneo ya kuingiilia mji wa Zanzibar na maeneo yenye taa za kuongezea magari.
Alizitaja Kampuni ya Raviltalco ya Romania na Rome Solutions iliyosajiliwa Zanzibar kuwa wamepewa kazi hiyo na zaidi ya kamera 900 zitafungwa katika maeneo hayo.
Alisema kampuni ya ZTE ya China imetoa kamera 10 kwa ajili ya kutunzia kumbukumbu na kuangalia matukio yanayochukuliwa na kamera na kampuni ya ZEST kwa kukshirikiana na Kampuni ya HUAWEI ya China wameahidi kuchangia vifaa vyenye thamani ya Dola za Marekani 20,000 ambavyo vinahusisha kamera 16 na mitambo yake.
Aliwaeleza waandishi wa habari kuwa ZTE baada ya kupata ombi la Makamu wa Pili wa Rais alipotembelea nchini China waliahidi kuongeza idadi ya kamera hadi kufikia 252.
Aliongeza kuwa pamoja na ufungaji wa kamera hizo, Serikali imeagiza vifaa vyengine vya kusaidia ulinzi katika maeneo ya nchi kavu na baharini na magari ya zimamoto.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara maalum alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanakuwa salama na biashara ya utalii inaimarika.
“Naomba niwahakikishie wananchi na wageni wetu kuwa Zanzibar ni eneo la usalama na litaendelea kuwa salama,” alisisitiza Waziri Haji Omar Kheir.
Akizungumzia madai ya baadhi ya wananchi kunyimwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi amesema hakuna mwananchi aliefika ofisini kwake kudai kunyimwa kitambulisho hicho isipokuwa kinachojitokeza ni malalamiko ya wanasiasa.
Aidha amepinga vikali juu ya kuhusishwa Kambi za Jeshi kutoa vitambulisho vya mzanzibari mkaazi na kusema kuwa hiyo sio kazi yao na vipo vyombo vilivyowekwa kisheria kufanya kazi hiyo.
No comments:
Post a Comment