MWENYEKITI wa Chama cha wananchi CUF, Prof Ibrahim Haruna Lipumba huenda akaingia kwa mara ya tano katika mbio za kutaka kuingia Ikulu ya Tanzania endapoUmoja wa Katiba ya WananchiUKAWA utampitisha kugombea Urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Lipumba ametangaza nia ya kugombea nafasi hiyo ya juu kisiasa nchini, akisema ana sifa zote lakini hatakuwa na kinyongo iwapo UKAWA haitapitisha jinalake kugombea urasi na atampigia kampeni atakaepitishwa.
Profesa Lipumba, anakuwa mwanasiasa wa tatu kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutangaza nia hiyo baada ya mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi na Dk George Kahangwa wa NCCR-Mageuzi kujitokeza kutaka kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano.
Mwanasiasa mwingine aliyejitokeza kuwania urais Tanzania ni Maxmillan Lyimbo wa TLP, wakati Hamad Rashid wa Alliance for Democratic Change (ADC) na Maalim Sharrif Hamad wa CUF wametangaza kuwania urais wa Zanzibar.
Lipumba, ambaye atakuwa akiwania urais kwa mara ya tano, iwapo atapitishwa na Ukawa ambayo imeamua kusimamia mgombea mmoja atakayeungwa mkono na vyama vinne, alitangaza nia yake juzi mjini Tabora wakati wa mikutano yake ya hadhara ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kupiga kura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25.
SOURCE:http://mrokim.blogspot.com/
No comments:
Post a Comment