Thursday, October 23, 2014

PATA HAPA NAKALA YA MUSWADA WA BARAZA LA VIJANA LA TAIFA; BORESHA TUPATE BARAZA BORA

indexKatika Mkutano wa 14 wa Bunge tarehe 21 Disemba 2013 ulisomwa Bungeni Muswada Binafsi wa Mbunge wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa wa mwaka 2013 niliouwasilisha tarehe 31 Oktoba 2013.
Narudia tena kuwashukuru vijana na wadau tulioshirikiana kuandaa muswada huo na naomba kuendelea kupata ushirikiano wenu wa karibu katika hatua zinazoendelea.
Kuanzia tarehe 21 Oktoba 2014 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii imeanza vikao vya kupokea maoni ya wadau kuhusu muswada huo. Nakala tete ya muswada huo inapatikana hapa, tafadhali pakua pitia na wasilisha maoni yako sasa. 
Unaweza kuandika maoni yako kwenye mtandao wa http://mnyika.blogspot.com au kutuma kwa barua pepe kwenda mbungeubungo@gmail.com na nakala kwa Kamati husika ya Bunge kupitia tanzparl@parliament.go.tz.
Ikiwa unataka kutumia njia nyingine kuwasilisha maoni yako tafadhali wasiliana na Gaston Garubimbi 0715/0767-825025 kwa maelezo zaidi. Mdau wa masuala ya vijana zingatia kwamba zaidi ya miaka 18 ahadi za kukamilisha mchakato wa kuanzishwa kwa baraza la Vijana la Taifa zimekuwa zikitolewa bila utekelezaji kamili na wa haraka. 
Baraza la Vijana la Taifa pamoja na malengo mengine litawezesha vijana kuanzia kwenye vijiji/mitaa mpaka taifa kuweza kuwa na vyombo vya kuwaunganisha vijana kwa kike na wa kiume kwa ajili ya maendeleo yao na ya taifa. 
Aidha, Baraza hilo litafuatilia pia kwa karibu utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya vijana kwenye Halmashauri, Serikali kuu, katika vyombo mbalimbali vya maendeleo na wadau wa maendeleo. 
Pia, Baraza la Vijana litafuatilia kwa karibu utendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kuhakikisha kwamba fedha zinatengwa za kutosha na kufika kwa walengwa kuwawezesha vijana kujiajiri, kukuza vipaji vyao na kushughulikia maendeleo yao kwa ujumla.
Kwa upande wangu nitashukuru ikiwa nitapokea maoni hayo kabla ya tarehe 28 Oktoba 2014, niweze kuyachambua na kutoa mrejesho mapema kuwezesha muswada kusomwa kwa mara ya pili Bungeni katika Mkutano wa 16 uliopangwa kuanza tarehe 3 Novemba 2014. 
Kwa mujibu wa Hansard tarehe 21 Disemba 2013 baada ya Muswada kusomwa kwa mara ya kwanza, Spika wa Bunge Anna Makinda alisema yafuatayo Bungeni “…muswada binafsi…. sasa utaanza kuwepo kwenye website ya Bunge na utakuwa public mpaka utakapopangiwa tarehe ya kujadiliwa na utapelekwa kwenye kamati zitakazohusika wakati muafaka”.
Majibu yanapaswa kutolewa na mamlaka husika ni kwanini toka wakati huo haukuwahi kuwekwa kwenye Tovuti ya Bunge pamoja na kukumbushwa. Hata hivyo nashukuru kuwa hatimaye sasa muswada huo umepelekwa kwenye Kamati, hivyo ni wakati muafaka kwa vijana na wadau wote kupata nakala ya muswada huo hapa na kutoa maoni ya kuboresha ili Baraza la Vijana la Taifa liweze kuundwa.
Kujadiliwa kwa muswada huo ni hatua ya pekee katika historia ya harakati za vijana nchini kwa kuzingatia kuwa Sera ya zamani ya maendeleo ya vijana ya mwaka 1996 ilitamka kwamba kutaanzishwa Baraza la Vijana na suala hilo kurudiwa katika Sera mpya ya mwaka 2007. 
Hata hivyo Serikali imekuwa ikikwepa kuhakikisha kwamba matakwa hayo ya sera tajwa yanatekelezwa kwa wakati pamoja na kuwa suala hilo linahusu mustakabali wa maendeleo ya vijana nchini. Hivyo pakua nakala pekua toa maoni; boresha muswada tupate baraza bora.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
23 Oktoba 2014

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...