Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Kyando Mchechu akitiliana saini na Kampuni ya Poly Technologies kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Valhalla, eneo la Masaki, Dar es Salaam. Shughuli ya utiaji saini imekuwa sehemu ya mkutano wa tatu wa uwekezaji kati ya Tanzania na China uliofanyika ukumbi wa mikutano wa nyumba ya wageni ya serikali ya Diaoyutai mjini Beijing, China.
Aidha, utiaji saini huo ambao utaziwezesha taasisi kadhaa za Tanzania kunufaika na mitaji na uwekezaji kutoka China ulikuwa sehemu ya ziara rasmi ya kiserikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Jakaya Kikwete China kwa mwaliko wa Rais Xi Jinping.
Mwandishi Maalumu,Beijing
Tanzania na China, zimetiliana saini mkataba wa maelewano (MoU) ambapo taasisi za China zitawekeza mabilioni ya dola za Marekani katika uchumi wa Tanzania.
Shughuli ya utiaji saini imekuwa sehemu ya mkutano wa tatu wa uwekezaji kati ya Tanzania na China uliofanyika ukumbi wa mikutano wa nyumba ya wageni ya serikali ya Diaoyutai mjini Beijing, China.
Aidha, utiaji saini huo ambao utaziwezesha taasisi kadhaa za Tanzania kunufaika na mitaji na uwekezaji kutoka China ulikuwa sehemu ya ziara rasmi ya kiserikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Jakaya Kikwete China kwa mwaliko wa Rais Xi Jinping.
Miongoni mwa makubaliano yaliyotiwa saini ni pamoja na ushirikiano wa kimkakati kati ya Shirika la Nyumba Tanzania (NHC) na kampuni ya China Railway Jianchang Engineering (CRJE) ambako kiasi cha dola bilioni moja unusu zitawekezwa katika uchumi wa Tanzania.
Kiasi cha dola bilioni moja zitawekezwa katika ujenzi wa mji mpya wa Salama Creek Satellite, eneo la Uvumba, wilaya ya Temeke, Dar es Salaam na kiasi cha dola milioni 500 zitawekezwa katika ujenzi wa Financial Square, eneo la Upanga.
Aidha, NHC itapata kiasi cha dola za Marekani milioni 200 kutoka kampuni ya Poly Technologies kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Valhalla, eneo la Masaki, Dar es Salaam.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pia limetiliana saini makubaliano na kampuni ya Hengyang Transformer ambapo kampuni hiyo itapata mamilioni ya dola za Marekani kwa ajili ya mradi wa kusambaza umeme vijijini.
Aidha, TANESCO limetiliana saini makubaliano ya ujenzi wa mradi wa umeme wa Kinyerezi IV.
Halmashauri ya manispaaa ya Temeke, Dar es Salaam imetiliana saini makubaliano na kampuni ya Jiangyin Tianhe Gasses Group ya ujenzi wa barabara ya lami ya Kikwete Friendship Highway katika wilaya ya Temeke.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Mecky Sadiq na Mkuu wa wilaya ya Temeke, Sofia Mjema, walishuhudia utiaji saini makubaliano hayo.
Vile vile, mkoa wa Pwani, umetiliana saini makubaliano na kampuni ya Jiansu Shenli Plastics Group Limited ya China kwa ajili ya kugharamia na kuendeleza mradi wa viwanda na uchumi katika eneo la Mlandizi.
Mkuu wa mkoa wa Pwani, Mwantumu Bakari Mahiza, alitia saini kwa niaba ya mkoa wake.
Wakati huo huo Rais Kikwete, alisema maendeleo ya haraka ya China ni hamasa kubwa na ya kutosha kwa nchi za Afrika kuwa nazo zinaweza kuendelea katika kipindi kifupi kama zitaongozwa na sera sahihi za mageuzi ya kiuchumi.
Rais Kikwete aliyasema hayo jana wakati alipokutana kwa mazungumzo rasmi na Mwenyekiti (Spika) wa Bunge la China, Zhang Dejiang, ikiwa ni moja ya shughuli za Rais katika ziara yake rasmi ya China.
Katika mazungumzo hayo kwenye jengo la Bunge la Great Hall of the People mjini Beijing, Rais Kikwete alimwambia Dejiang: “China inatuhamasisha kwamba na sisi tunaweza kupata mabadiliko na maendeleo ya haraka ya wananchi wetu ili mradi tu tuweze kuwa na sera sahihi ambazo zinalenga katika kuleta mageuzi ya msingi na ya kweli kweli ya kiuchumi”.
Alisema kwake yeye ambaye amekuwa anatembelea China kila baada ya wastani wa miaka minne, mabadiliko ya China yanatia hamasa kweli kuwa nchi za Afrika pia zinaweza kuleta mageuzi makubwa ya maisha ya watu wake.
“Nilikuja hapa kwa mara ya kwanza mwaka 1980, na tokea wakati huo nimetembelea nchi hii kila baada ya miaka minne kwa wastani na kila nikija nashuhudia mabadiliko makubwa yasiyopimika na wala kufikirika. China ilikuwa nchi masikini sana wakati nilipofika hapa kwa mara ya kwanza lakini katika miaka 30 tu imebadilika kutoka nchi masikini na kuwa nchi iliyoendelea na yenye uchumi unaoshikilia nafasi ya pili kwa ukubwa duniani,” alisema.
“Tunawapongeza kwa juhudi ambazo zimewafikisheni hapa. Mnatuhamasisha na sisi kuwa ipo siku moja na sisi katika Afrika tutafikia hatua hii ya maendeleo,” alisema.
Naye Dejiang alimkubusha Rais Kikwete mazungumzo kati yao wakati walipokutana kwa mara ya kwanza miaka saba iliyopita Ikulu, mjini Dar es Salaam.
Wakati huo, Dejiang alikuwa Katibu wa Chama Tawala cha Kikomunisti cha China katika jimbo la Guangzhou, jimbo ambalo linaongoza katika China kwa kufanya biashara na Tanzania.
Kati ya biashara zote ambazo Tanzania na China zinafanya, asilimia 60 inatokea jimbo la Guangzhou.
Alipongeza uhusiano mzuri kati ya Tanzania na China katika miaka 50 tokea nchi hizo mbili kuanzisha uhusiano wa kibalozi Aprili 26, mwaka 1964.
Pia alisema ujenzi wa Reli ya TAZARA unaendelea kuthibitisha urafiki baina ya watu wa China, Tanzania na Zambia na kuongeza kwa Tanzania kwa kuimarisha TAZARA na kwa kutilia maanani utajiri na raslimali zilizopo, ikiwemo nafasi ya kijiografia, utulivu na amani na idadi kubwa ya watu, Tanzania ina sifa ya kuwa nchi tajiri katika miaka isiyokuwa mingi ijayo.
No comments:
Post a Comment