Na Mwandishi Wetu, Shinyanga
Benki ya Exim imesaini makubaliano ya kuifadhili timu ya mpira wa miguu ya Stand United FC ya mkoani Shinyanga. Hii ni timu ya kwanza kupata ufadhili toka Benki ya Exim. Ufadhili huo wa mwaka mmoja utaisaidia timu hiyo kushiriki katika ligi kuu soka Tanzania bara kwa msimu wa 2014/2015.
“Makubaliano haya yanaikutanisha Benki ya Exim na mchezo mkubwa kuliko yote Tanzania,” alisema mkuu wa matawi ya Benki ya Exim kanda ya ziwa, Bw. Justus Mukurasi jana katika hafla fupi iliyofanyika mkoani Shinyanga. Aliongeza kuwa hakuna mchezo wenye watazamaji, wafuatiliaji na mashabiki wengi zaidi nchini kama mpira wa miguu.
“Timu ya Stand United inanguvu kubwa ya kuunganisha mashabiki wa kanda ya ziwa. Hivyo ni jambo stahiki kwa Benki ya Exim kuisaidia timu hii ambayo mashabiki wake ni miongoni mwa wateja wa Benki ya Exim,” alisema Bw. Mukurasi.
Mukurasi aliongeza kuwa pande hizo mbili zilifanikiwa kuingia katika makubaliano ambayo yataiwezesha benki hiyo kuifadhili timu ya Stand United toka Ligi Kuu Tanzania bara ilipoanza.
“Kwetu sisi udhamini tuliofanya sio tu wa nembo, nbali ni ufadhili wa muda mrefu utakaozinufaisha pande zote mbili,” alisema Mukurasi.
”Tunatumai kuwa kila mmoja wetu ataweza kujifunza kutoka kwa mwenzake ili kupata matokeo mazuri kwa pamoja. Exim itasaidia kukuza na kuundeleza mchezo wa soka na hivyo kuiwezesha benki yetu karibu zaidi na wateja wake,” alisema Bw. Mukurasi.
Naye, Mwenyekiti wa Stand United FC, Bw. Aman Vicent alisema kuwa timu yake inayofuraha kubwa kuingia katika makubaliano na Benki ya Exim. “Tunadhamiria kuimarisha uhusiano huu ili kuhakikisha timu yetu inafanya vizuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu,” alisema Bw. Vicent.
“Kwa niaba ya Stand United FC, ningependa kuishukuru Benki ya Exim kwa jitiada zao za kusaidia wachezaji wetu na timu kwa ujumla. Tunafanya kazi kubwa kuhakikisha tunainua vipaji vya wachezaji wetu ili na wao waweze kufika mbali zaidi,” aliongeza Bw. Vicent.
No comments:
Post a Comment