Friday, February 07, 2025

Wananchi Ntunduwaro wanufaika na Makaa ya Mawe




-      Wajengewa barabara, Zahanati

-      MILCOAL yatoa fursa za ajira


UZALISHAJI   wa madini ya makaa ya mawe katika kijiji cha Ntunduwaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga  ni  chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali na  maendeleo  ya wananchi wa kata hiyo.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Meneja wa mgodi wa Market Insight Limited (MILCOAL),  Atit Mehta amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024 mgodi huo umeweza  kuilipa serikali Shilingi  Bilioni 5.2 kutokana na mrabaha, tozo na ada mbalimbali.

Kuhusu Kampuni hiyo kuwajibika kwa jamii inayozunguka mradi kwa maana ya CSR, Mehta amesema wamekuwa wakitekeleza kwa uaminifu  Sera ya Madini inayotambua uwajibikaji wa Kampuni  kwa jamii zinazozunguka miradi na mgodi wao wameweza kujenga barabara ya kutoka Ntunduwaro mpaka Liyumbi yenye urefu wa Kilomita 23.

“Kwa sasa tunamalizia mchakato wa mwisho na viongozi wa Serikali akiwemo Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO) tuweze kujenga Zahanati Ntunduwaro ili kuleta unafuu wa matibabu kwa wananchi wa  kijiji hiki,”amesema.

Aidha  amesema, pia kampuni hiyo ya MILCOAL imetoa ajira kwa watu 200 kati yao tisa ni wenye asili ya Kihindi na waliosalia ni wazawa.

Nae, Mjiolojia Abraham Nkya akizungumza kwa niaba ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, amesema mgodi huo wa MILCOAL ambao upo mkoani Njombe ukiwa unapakana na wilaya ya Mbinga ndio unaochangia kiasi kikubwa cha mapato ya Serikali katika Sekta ya Madini kwenye  mkoa huo.

“Madini ya Makaa ya Mawe ndio yanayoongoza kwa kutupa  mapato makubwa, mwaka wa fedha uliopita wa 2023/2024  madini ya makaa ya mawe pekee yaliingiza  kiasi cha shilingi bilioni  4.155  na kuufanya Mkoa wa Njombe kuchangia vizuri mapato ya Serikali,”amesema.

Kwa upande wa Mjiolojia kutoka MILCOAL, Cyprian Ndaza ametoa wito kwa Serikali kuendelea kuweka mazingira mazuri zaidi kwa wawekezaji ili ajira zaidi ziweze kutolewa kwa wazawa.



No comments:

Wananchi Ntunduwaro wanufaika na Makaa ya Mawe

-      Wajengewa barabara, Zahanati -      MILCOAL yatoa fursa za ajira UZALISHAJI   wa madini ya makaa ya mawe katika kijiji cha Ntunduwaro...