Dodoma, Februari 5, 2025 – Mgombea Mteule wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Mgombea Mwenza wake, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, wametambulishwa rasmi kwa wananchi na wanachama wa chama hicho katika maadhimisho ya miaka 48 ya CCM yaliyofanyika leo katika Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, pamoja na maelfu ya wanachama wa CCM kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania. Katika hotuba yake, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewashukuru viongozi wa chama kwa imani waliyompa na kuahidi kuendelea kuwatumikia Watanzania kwa moyo wa uadilifu, kujituma, na uwajibikaji mkubwa.
“Ninayo heshima kubwa kwa heshima hii mlionipa. Naahidi kuendelea kusimamia misingi ya haki, maendeleo, na ustawi wa wananchi wote,” alisema Dkt. Samia huku akishangiliwa na umati mkubwa wa wananchi waliojitokeza kushiriki maadhimisho hayo.
Kwa upande wake, Mgombea Mwenza, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, alisisitiza mshikamano na umoja wa Watanzania huku akiahidi kushirikiana kwa karibu na Dkt. Samia katika kuleta maendeleo kwa Taifa.
“Tutaendelea kushirikiana na kila Mtanzania katika kuhakikisha nchi yetu inapiga hatua zaidi za maendeleo. Umoja wetu ndio silaha yetu kubwa,” alisema Dkt. Nchimbi.
Sherehe za maadhimisho ya miaka 48 ya CCM zimeambatana na burudani mbalimbali, ngoma za asili, nyimbo za hamasa, pamoja na hotuba kutoka kwa viongozi wa chama, huku wananchi wakionyesha furaha na matumaini makubwa kwa uongozi unaokuja.
No comments:
Post a Comment