Goalkeeper Award
Dodoma, Tanzania – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma akipokelewa kwa heshima kubwa na viongozi wa serikali, wananchi, na wadau mbalimbali baada ya kutunukiwa Tuzo Maalum ya Kimataifa ya The Global Goalkeeper Award.
Tuzo hiyo, inayotolewa na Wakfu wa Bill & Melinda Gates, inatambua mchango mkubwa wa Rais Samia katika kusukuma mbele maendeleo endelevu, hususan katika nyanja za afya, elimu, na uwezeshaji wa wanawake na vijana.
Mara baada ya kuwasili, Rais Samia alipokelewa kwa shangwe huku wananchi wakionesha furaha na fahari kwa heshima hiyo kubwa aliyopata kiongozi wao. Viongozi mbalimbali wa kitaifa, wakiwemo Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, na wabunge, walijumuika kumpokea na kutoa pongezi kwa mafanikio hayo makubwa.
Akizungumza mara baada ya kuwasili, Rais Samia alieleza kuwa tuzo hiyo si yake binafsi bali ni ya Watanzania wote, akisisitiza kuwa jitihada za pamoja katika maendeleo ya jamii ndiyo zimeiwezesha Tanzania kupata heshima hiyo kimataifa.
Tuzo ya The Global Goalkeeper Award hutolewa kila mwaka kwa viongozi wa dunia wanaoonyesha mchango mkubwa katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa. Ushindi wa Rais Samia ni ishara ya kutambuliwa kwa juhudi za Tanzania katika kuboresha ustawi wa jamii na kuleta maendeleo jumuishi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment