Saturday, February 01, 2025

TEA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA MAFUNZO YA AMALI

Mkurugenzi Mkuu wa TEA Dkt. Erasmus Kipesha (wa pili kushoto) akifurahia jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya TEA Dkt. Leonard Akwilapo walipokutana kwenye maonesho ya uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo Jijini Dodoma. Kulia ni Bw. Godfrey Boniventure mjumbe wa Bodi ya TEA na kushoto ni CPA. Mwanahamis Chambega Kaimu Mkurugenzi huduma za taasisi TEA
Mjumbe wa Bodi ya TEA Bw. Godfrey Boniventure akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la TEA kwenye maonesho ya uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo jijini Dodoma
Mkurugenzi Mkuu wa TEA Dkt. Erasmus Kipesha akizungumza na vyombo vya habari kuhusu uboreshaji wa miundombinu ya elimu kwa ajili ya kutekeleza Sera mpya ya Elimu na Mafunzo jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dkt. Erasmus Kipesha akiwa kwenye picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bodi, Mjumbe wa Bodi pamoja na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti wa TEA walipokuwa kwenye uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo jijini Dodoma.


Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imejipanga kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia mafunzo ya amali kama sehemu ya kuunga mkono utekelezaji wa Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya uzinduzi wa Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 Toleo la 2023, Jijini Dodoma Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dkt. Erasmus Kipesha, amesema jukumu la TEA ni kusimamia uboreshaji wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia, huku akisisitiza kuwa utekelezaji wa sera mpya ya elimu unahitaji miundombinu imara na vifaa vya kutosha kwa ajili ya mafunzo ya amali.

Dkt. Kipesha ameeleza kuwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi haiwezi kutekelezwa kwa ufanisi bila kuboresha miundombinu, hivyo TEA ina jukumu kubwa la kuhakikisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia yanaboreshwa kwa viwango vinavyohitajika.

Ameongeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha, takribani shilingi bilioni 3 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na uboreshaji wa miundombinu katika shule 20, zinazotoa mafunzo ya amali kwenye fani za kilimo, TEHAMA, mapishi, ushonaji, michezo, na sanaa.

Katika kutekeleza Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, TEA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu kutafuta rasilimali fedha ili kuhakikisha miundombinu ya mafunzo ya amali inaboreshwa na vifaa vinapatikana kote nchini.

 

No comments:

CCM ARUSHA WAUNGA MKONO AZIMIO, RAIS SAMIA NA RAIS MWINYI WAGOMBEA PEKEE 2025

  Na Vero Ignatus,Arusha MAELFU ya Wananchi wa Mkoa wa Arusha leo Jumamosi Februari 1, 2025 wamejitokeza kwa wingi kwenye tukio la kuung...