Vijana Watakiwa Kuwa Waaminifu katika Kazi
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira kwa wachimbaji wadogo wa madini kwa kuhakikisha wanapata mitaji, leseni, na teknolojia ya kisasa katika shughuli za uchimbaji. Hatua hizi zimewasaidia wachimbaji wadogo kuchimba kwa tija na kunufaika zaidi na sekta ya madini.
Akizungumza katika mahojiano maalum, mmiliki wa Mgodi wa Kwasakwasa uliopo katika kijiji cha Msesule, kata ya Mapogoro, wilayani Mbarali, mkoani Mbeya, Bi. Amagite Mkumbwike amepongeza jitihada za Serikali katika kuweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wadogo.
"Serikali ya Awamu ya Sita imeweka mazingira bora kwa wachimbaji wadogo, ikiwemo kuhakikisha bei nzuri ya dhahabu sokoni ili tuweze kunufaika zaidi. Kama mchimbaji mdogo na mmiliki wa mgodi wa Kwasakwasa, nitaendelea kumuunga mkono Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kutoa ajira kwa vijana na kurejesha faida kwa jamii inayozunguka mgodi wetu," alisema Bi. Amagite.
Aliongeza kuwa kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa na Serikali, wameweza kurejesha sehemu ya faida kwa jamii kwa kununua vifaa vya shule kwa wanafunzi wanaotoka katika kijiji hicho na wanaoendelea na masomo ya elimu ya juu, pamoja na kununua mashine ya umwagiliaji ili kusaidia shughuli za kilimo katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Msimamizi wa mgodi huo, Bw. Edward Daud, ameiomba Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kutoa fursa zaidi za ajira kwa vijana.
"Tunaomba Serikali iendelee kuweka mazingira rafiki zaidi kwa wawekezaji ili vijana wengi wapate ajira kutokana na uwekezaji unaofanywa katika sekta hii. Pia, nawasihi vijana tujitume kwa bidii na kuwa waaminifu katika kazi tunazopewa. Tukiwa waaminifu na kufanya kazi kwa ufanisi, tutasaidia kuimarisha sekta ya madini na kukuza uchumi wa nchi yetu," alisema Bw. Edward.
Serikali imeendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya madini kuhakikisha kuwa wachimbaji wadogo wanakuwa na nyenzo sahihi za kufanya shughuli zao kwa ufanisi, huku ikisisitiza umuhimu wa wachimbaji wadogo kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa kwa maendeleo endelevu ya sekta hiyo.
No comments:
Post a Comment