Thursday, February 06, 2025

AGA KHAN 'V' ACHUKUA UONGOZI WA IMAMAT, AKITHIBITISHA AHADI YA KUENDELEZA MAENDELEO TANZANIA, AFRIKA NA DUNIANI NZIMA

 


Prince Rahim Al-Hussaini pichani ameteuliwa kuwa Imam wa 50 wa Madhehebu ya Ismailia.

JUMUIYA ya Waislamu wa Kisheia Ismaili imemtangaza Prince Rahim Aga Khan V kama Imamu wa 50 wa urithi wa Waislamu wa Kisheia Ismaili, kufuatia kifo cha baba yake Aga Khan IV, aliyefariki dunia mjini Lisbon akiwa na umri wa miaka 88.

Mpito huu unaendeleza ahadi ya kudumu ya Imamu wa Ismaili kwa maendeleo ya kibinadamu, ambayo imekuwa nguzo muhimu ya kazi iliyofanywa chini ya uongozi wa Aga Khan IV ambaye katika uongozi wake wa miongo kadhaa, alijitolea kuboresha hali ya maisha duniani kote, kwa msisitizo maalum barani Afrika, Asia, na maeneo mengine yanayohitaji miradi ya maendeleo.

Kupitia Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), aliongoza upanuzi wa miradi inayolenga kuimarisha elimu, huduma za afya, maendeleo ya uchumi, na uhifadhi wa utamaduni katika mabara mbalimbali Afrika, hususan Tanzania, Kenya, Uganda, na Msumbiji, imekuwa eneo la kipaumbele kwa uwekezaji mkubwa katika shule, vyuo vikuu, hospitali, huduma za kifedha, na maendeleo endelevu yanayolenga kuleta mabadiliko ya muda mrefu.

Dira ya Kuendeleza na Kupanua Miradi
Chini ya uongozi wa Aga Khan V, Imamu wa Ismaili amethibitisha dhamira yake ya kuhakikisha kuwa miradi na programu zote zilizoanzishwa na Aga Khan IV zinaendelea na kuimarishwa zaidi.

"Kwa muda mrefu, Prince Rahim Aga Khan V amehusika kikamilifu katika uongozi wa AKDN, akiwa na mchango mkubwa katika mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, uhifadhi wa mazingira, na kupunguza umaskini".

Uwepo wa AKDN nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla unasalia kuwa sehemu kuu ya dhamira yake, kupitia miradi inayoendelea ambayo inajumuisha:

Kuongeza upatikanaji wa elimu bora kupitia Shule za Aga Khan na vyuo vikuu vya Aga Khan Afrika Mashariki, kuimarisha mifumo ya afya na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za kisasa za tiba kupitia Aga Khan Health Services (AKHS).

Miradi mingine ni kuhamasisha maendeleo ya uchumi kwa kusaidia ujasiriamali na miradi ya kifedha kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Aga Khan (AKFED) na kuimarisha uendelevu wa mazingira, kwa kuendeleza miundombinu rafiki kwa mazingira na programu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Jumuiya ya Ismaili inaposherehekea urithi wa Aga Khan IV, Imamat inaingia katika enzi mpya ya uongozi, ikiendeleza ahadi yake ya kuimarisha maendeleo ya kijamii, ustawi wa binadamu, na maendeleo endelevu kwa jamii zinazoihitaji zaidi.

Prince Rahim Aga Khan V ni mtoto wa kwanza wa Aga Khan IV, Amezaliwa tarehe 12 Oktoba 1971, amesoma katika Phillips Academy Andover na Chuo Kikuu cha Brown, na amehudumu katika bodi mbalimbali za AKDN, akiongoza pia Kamati ya Mazingira na Tabianchi, kwa kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inaendana na malengo ya uendelevu wa muda mrefu.

No comments:

WAZIRI NA NAIBU WAZIRI WA ARDHI WASHIRIKI MKUTANO WA BUNGE KWA AJILI YA KUWASILISHA TAARIFA ZA SHUGHULI ZA KAMATI

  Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi, pamoja na Naibu Waziri, Mhe. Geophrey Pinda, wameshiriki Mkutano...