Thursday, February 06, 2025

SERIKALI YAPITIA MAREKEBISHO YA SHERIA NA MKAKATI WA PPP KUIMARISHA UBIA KATIKA MAENDELEO

 






Picha ya Pamoja ya baadhi ya wajumbe walioshiriki kikao kazi cha kupitia Marekebisho ya sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), pamoja na kupitia utekelezaji wa Mkakati wa miaka mitano wa Sera ya Taifa ya PPP iliyofanyika jijini Dar es Salaam. 
*****************  
Na. Eva Ngowi -WF -Dar es Salaam 
Wizara ya Fedha kupitia Kitengo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi – PPP imefanya kikao kazi cha kupitia Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi (PPP), pamoja na kupitia utekelezaji wa Mkakati wa Miaka Mitano wa Sera ya Taifa ya PPP. 
 
Hayo yameelezwa na Kaimu Kamishna wa Kitengo cha PPP, Bw. Bashiru Taratibu wakati akifungua kikao kazi hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Hazina Ndogo jijini Dar es Salaam.
 
Bw. Taratibu alisema kuwa lengo la kikao kazi hicho lilikuwa kupitia utekelezaji wa Mkakati wa Sera ya Taifa ya PPP na maboresho ya Sheria ya PPP, Sura 103 iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kuona changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wake ili wakati wa kufanya maboresho waweze kubaini maeneo yenye changamoto katika utekelezaji ili yaweze kupatiwa ufumbuzi katika utekelezaji ujao.  
 
“Kikao kazi hiki kinahusu masuala yote ya Kisera, Sheria na Kanuni leo tumewaita wenzetu wa Wizara mbalimbali na Taasisi zilizo chini yao kwa ajili ya kuja kupitia Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya PPP ulioandaliwa mwaka 2021, ni Mkakati wa Miaka Mitano wa mwaka 2021/22- 2025/26 kwa hiyo sasa hivi tunakaribia mwisho wa Mkakati huo lakini katika ujio wetu wa leo na katika siku hizi tano tutakazofanya kikao kazi hiki katika ngazi ya Wizara tutapitia Mkakati huo kuona utekelezaji wake, kukumbushana majukumu ya kila mdau kwenye ule Mkakati” Alisema Bw. Taratibu.
 
Alisema kuwa vile vile mwaka 2023 walifanya marekebisho ya Sheria, na kwamba yale marekebisho pia wamekuja kukumbushana na kujulishana kuwa marekebisho hayo ni yapi, ili hizo Wizara ambazo ndio zenye majukumu mbalimbali ambayo yanatekelezwa na Taasisi zao ziyaelewe na kutumia vizuri fursa zinazopatikana kupitia dhana ya PPP.
 
Aidha, Bw. Taraibu alisema kuwa pamoja na kupitia marekebisho ya Mkakati, pia aliwafahamisha moja ya jukumu la PPP kuwa ni kuishirikisha Sekta Binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo huko nyuma yalikuwa ni majukumu ya Serikali.
 
“Tunaamini wenzetu hawa ambao wengi wametoka katika Wizara mbalimbali wakiielewa hii dhana vizuri ina maana kuwa yale majukumu ambayo yanauwezo wa kutekelezwa kwa kutumia Sekta Binafsi watahakikisha kuwa yanakwenda kutekelezwa kwa kuishirikisha Sekta binafsi, jambo ambalo ndiyo madhumuni makubwa ya Sera” alisema Bw. Taratibu. 
 
Kikao kazi hicho kimeshirikisha baadhi ya Wizara ambazo zina miradi ya maendeleo hasa miradi ya masuala ya miundombinu kama vile Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Afya.

No comments:

WAZIRI NA NAIBU WAZIRI WA ARDHI WASHIRIKI MKUTANO WA BUNGE KWA AJILI YA KUWASILISHA TAARIFA ZA SHUGHULI ZA KAMATI

  Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi, pamoja na Naibu Waziri, Mhe. Geophrey Pinda, wameshiriki Mkutano...