Saturday, February 08, 2025

VIONGOZI WA EAC NA SADC WAJADILI HALI YA USALAMA DRC, WATAKA SULUHISHO LA KUDUMU




















Dar es Salaam, Februari 8, 2025 – Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamekutana Ikulu jijini Dar es Salaam kujadili hali ya usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wakisisitiza kuwa mgogoro huo unahitaji suluhisho la kudumu kwa njia za mazungumzo na mshikamano wa mataifa ya Afrika.

Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alieleza kuwa nchi wanachama haziwezi kukaa kimya wakati raia wasio na hatia wanaendelea kupoteza maisha.

"Sote tunafahamu kwamba DRC bado inakabiliwa na migogoro. Kama viongozi, hatuwezi kukaa kimya. Nchi zetu zina wajibu wa kuhakikisha tunashughulikia changamoto hii ambayo inaathiri watu nchini humo," alisema Rais Samia.

Akitilia mkazo umuhimu wa mshikamano wa Kikanda, Rais Samia alisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kusaidia masuala ya kidiplomasia ili kuhakikisha mgogoro huo unapata suluhisho la kudumu.

Kwa upande wake, Rais wa Kenya, ambaye pia ni Mwenyekiti wa EAC, Mhe. William Samoei Ruto, alikemea matumizi ya silaha kama njia ya kutatua mgogoro huo na kusisitiza umuhimu wa mazungumzo na mashauriano.

"Mgogoro huu hautaweza kusuluhishwa kwa njia za kijeshi. Lazima tukatae kupiga mabomu, badala yake tuwekeze kwenye suluhu za kidiplomasia kwa kushirikisha wadau wote," alisema Rais Ruto.

Aliongeza kuwa hatua za haraka zinahitajika ili kuokoa mamilioni ya watu wanaokimbia vita, akionya kuwa hali hiyo inazidi kuleta athari kubwa kwa ukanda mzima wa Afrika na dunia kwa ujumla.

Naye Rais wa Zimbabwe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa SADC, Mhe. Emerson Dambudzo Mnangagwa, alihimiza mshikamano wa mataifa ya Afrika katika kusimamia amani, akilinganisha hali ya sasa na kipindi cha harakati za ukombozi wa Bara la Afrika.

"Kinachoendelea DRC kina madhara makubwa si kwa nchi hiyo pekee, bali kwa bara zima la Afrika. Tunapaswa kushikamana kama tulivyofanya wakati wa kupigania uhuru," alisema Rais Mnangagwa.

Viongozi hao walikubaliana kuwa umoja, mshikamano na juhudi za kidiplomasia ndizo zitakazosaidia kuleta suluhisho la kudumu katika mgogoro wa DRC, huku wakihimiza kuwa Afrika inapaswa kuchukua hatua madhubuti pasipo kusubiri uingiliaji wa mataifa ya nje.

No comments:

VIONGOZI WA EAC NA SADC WAJADILI HALI YA USALAMA DRC, WATAKA SULUHISHO LA KUDUMU

Dar es Salaam, Februari 8, 2025 – Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamekut...