Saturday, February 01, 2025
CCM ARUSHA WAUNGA MKONO AZIMIO, RAIS SAMIA NA RAIS MWINYI WAGOMBEA PEKEE 2025
Na Vero Ignatus,Arusha
MAELFU ya Wananchi wa Mkoa wa Arusha leo Jumamosi Februari 1, 2025 wamejitokeza kwa wingi kwenye tukio la kuunga Mkono azimio la Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi la Januari 19, 2025 lililomuidhinisha Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Dkt. Hussein Mwinyi wa Zanzibar, kuwa wagombea Urais kupitia CCM katika Uchaguzi mkuu wa baadae mwaka huu.
Chama Cha Mapinduzi CCM mkoa wa Arusha leo Jumamosi wamefanya Mkutano Mkubwa wa hadhara kwenye viwanja vya Kilombero Jijini Arusha ili kuunga Mkono azimio hilo, wakati huu ambapo Chama hicho tawala kikiendelea na shamrashamra za kuelekea miaka 48 ya kuzaliwa kwake.
Kilimanjaro Marathon yaongeza muda wa kuchukua nambari za ushiriki
Na mwandishi Wetu, Michuzi Tv
WAANDAJI wa Mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon 2025 wametangaza kuongeza muda wa washiriki kuchukua nambari zao za ushiriki pamoja na T-shirts za ushiriki, zoezi linalotarajiwa kuanza katika kipindi cha wiki mbili zijazo Jijini Dar es Salaam.
Zoezi hilo linatarajiwa kuanza rasmi baada ya kufungwa kwa zoezi la kujiandilisha ili kushiriki mbio hizo kukamilika, ambapo idadi iliyokuwa imewekwa ya washiriki katika mbio za kilomita 42 na zile za kilomita 21 tayari zimejaa hata kabla ya Februari 6, mwaka huu, tarehe ambayo ilikuwa imewekwa kama siku ya kufunga zoezi la kujiandikisha kushiriki.
"Tumeongeza muda wa kukusanya nambari hizo na T-shirts hadi nyakati za jioni ili wale wanaotoka kazini nyakati hizo waweze kuchukua nambari zao Jijini Dar es Salaam na Arusha ili kupunguza msongamano wa dakika za mwisho mjini Moshi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na waandaaji, zoezi la ukusanyaji wa nambari hizo utaanza rasmi Ijumaa Februari 14, 2025 katika ukumbi wa Mlimani City Mall (mbele ya Samaki Samaki) kuanzia saa 10 alasiri hadi saa moja za jioni ambapo siku ya Jumamosi Februari 15 na Jumapili Februari 16, zoezi hilo litaanza saa nne (4) asubuhi hadi saa 12 za jioni.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, zoezi hilo litahamia Jijini Arusha Jumanne ya Februari 18 na Jumatano Februari 19, ambapo ukusanyaji wa nambari hizo utafanyika katika hoteli ya Kibo Palace kuanzia saa kuanzia saa 8 mchana hadi za moja ya jioni.
Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa sehemu ya mwisho ya ukusanyaji wa nambari itakuwa ni mjini Moshi siku ya Alhamisi Februari 20 kuanzia saa 6 za mchana hadi saa 11 jioni, Ijumaa Februari 21 kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 12 za jioni na Jumamosi Februari 22 kuanzia saa 4 asubuhi hadi s11 jioni, zoezi ambalo litafanyikia uwanja wa michwezo wa chuo kikuu cha Uhsirika Moshi (MoCU).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya waandaaji, nambari za Mbio za kilomita 5 zinazofadhiliwa na benki ya CRDB bado zinaendelea kuuzwa ambapo wanaotarajiwa kushiriki wanaweza kujiandikisha kupitia Mixx by YAS (zamani Tigopesa) kwa kupiga *150*01#, kisha kubonyeza 5 LKS, kisha kubonyeza 6 (Tiketi) na kufuata maelekezo ili kukamilisha usajili wao au mtandaoni kupitia www.kilimanjaromarathon.com. Aidha wanaotarajia kushiriki wamekumbushwa ya kuwa kuna idadi ndogo katika mbio hizo pia na tayari asilimia 60 ya nafasi hizo tayari zimeshachukuliwa.
Aidha waandaaji hao wamewataka washiriki hao kuzingatia nyakati zilizotangazwa ili kuepuka usumbufu na pia wametoa wito kwa wale wanaokusanya nambari kwa ajili ya marafiki au ndugu zao kuhakikisha wanakuwa na nakala za vitambulisho vya wanaowachukulia pamoja na barua za ridhaa zinazowaruhusu wawakilishi wao kuchukua kwa niaba yao
Waandalizi hao pia walitoa onyo kali dhidi ya wale wanaouza nambari mtandaoni kinyume cha sheria wakisema kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. "Hii ni kinyume cha sheria na tutawachukulia hatua za kisheria," waandaaji walisema.
Pia imewaonya wale wanaotarajia kukimbia na nambari zisizo rasmi (nambari feki) ambapo wale watakaobainika kufanya hivyo wataondolewa kwenye orodha ya ushiriki na kufungiwa kushiriki mbio Kilimanjaro International Marathon.
Waandaaji hao pia walisema kuwa mbio hizo ni tukio muhimu na kwamba wandaaji hawatavumilia wale watakaokiuka kwa njia moja au nyingine kanuni za mbio hizo ikiwemo ya kufanya jambo lolote lile ambalo litaweza kuathiri au kuleta mgongano wa kimaslahi kwa wadhamini wa mbio hizo ambao ni Kilimanjaro Premium Lager Marathon, Yas Kili Half Marathon na CRDB Bank Fun Run.
Wadhamini wa mwaka huu ni pamoja na wadhamini wakuu Kilimanjaro Premium Lager ambao wanadhamini mbio za kilomita 42, wadhamini wa kilomita 21 YAS, wadhamini wa mbio za kujifurahisha za kilomita 5 benki ya CRDB Bank, pamoja na wadhamini wengine wa meza za maji ni Simba Cement, Kilimanjaro Water, TotalEnergies na TPC Sugar, pamoja na washirika rasmi-GardaWorld Security, CMC Motors, Hoteli za Salinero –Kilimanjaro na wasambazaji rasmi Kibo Palace Hotel na Keys Hotel.
Kili Marathon huandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa hapa nchini na kampuni ya Executive Solutions Limited.
TEA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA MAFUNZO YA AMALI
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imejipanga kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia mafunzo ya amali kama sehemu ya kuunga mkono utekelezaji wa Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya uzinduzi wa Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 Toleo la 2023, Jijini Dodoma Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dkt. Erasmus Kipesha, amesema jukumu la TEA ni kusimamia uboreshaji wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia, huku akisisitiza kuwa utekelezaji wa sera mpya ya elimu unahitaji miundombinu imara na vifaa vya kutosha kwa ajili ya mafunzo ya amali.
Dkt. Kipesha ameeleza kuwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi haiwezi kutekelezwa kwa ufanisi bila kuboresha miundombinu, hivyo TEA ina jukumu kubwa la kuhakikisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia yanaboreshwa kwa viwango vinavyohitajika.
Ameongeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha, takribani shilingi bilioni 3 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na uboreshaji wa miundombinu katika shule 20, zinazotoa mafunzo ya amali kwenye fani za kilimo, TEHAMA, mapishi, ushonaji, michezo, na sanaa.
Katika kutekeleza Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, TEA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu kutafuta rasilimali fedha ili kuhakikisha miundombinu ya mafunzo ya amali inaboreshwa na vifaa vinapatikana kote nchini.
DC MPOGOLO USAFI ZOEZI LA KUDUMU ILALA
Katika kuhakikisha zoezi la usafi linakua la kudumu, Mkuu wa wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amewataka wananchi, wafanyabiashara na taasisi zote ndani ya halmashauri hiyo kufanya usafi kuwa zoezi la kudumu.
Mkuu huyo wa wilaya ya Ilala ameyazungumza hayo wakati wa zoezi maalum la usafi lililofanyika february mosi 2025.
Mpogolo amesema mkakati wa Ilala ni kwa Kanda namba 1 na 2 za Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam kuanzia eneo la Kamata, Mtaa wa Gerezani kupitia barabara ya Sokoine, Kivukoni front, Luthuli, barabara ya Barack Obama kuelekea fukwe za Dengue kufanyike usafi wa kila mara.
Amesema ili zoezi ilo liwe endelevu kwa kila mwananchi, taasisi, wafanyabiashara na wadau wengine waweke utaratibu wa usafi kila siku kabla na baada ya kuanza na kumaliza shughuli zao wahakikishe mazingira yanakua safi.
Mpogolo amebainisha viongozi wamekubaliana kulifanya Jiji la Ilala kuendeleza usafi wa mazingira, taasisi, makazi na fukwe zote kuendelea kuwa safi.
Mpogolo amesisitiza zoezi la usafi kwa sasa katika wilaya ya Ilala ni la kila siku, huku zoezi la usafi wa pamoja la kila mwisho wa mwezi litaendelea ikiwa ni pamoja na kampeni za usafi za kila mara kuweka jiji safi.
Aidha Mpogolo ametoa wito kwa Wananchi, Taasisi na wadau mbalimbali wa mazingira kujitokeza katika mazoezi ya usafi endelevu ili kuhakikisha jiji la Ilala linaendelea kuwa safi kwa jitihada za pamoja kutokomeza uchafu na magonjwa ya mlipuko.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam amesema ofisi yake itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kufanyia usafi vinapatikana katika mazoezi hayo kwa kushirikiana na Wakandarasi wa usafi wanaofanya kazi ndani ya jiji la Ilala.
Mkutano wa 19 wa ACA Kufanyika Dar es Salaam 2025, Kuangazia Uwekezaji katika Sekta ya Korosho
Mkutano huo umendaliwa na Jukwaa la Korosho Afrika (ACA) kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho Tanzania na Umoja wa Wabanguaji Wakubwa wa Korosho Tanzania (TACP).
Pia Mkutano wa 19 wa Mwaka wa ACA unakusudiwa kuhudhuriwa na washiriki wasiopungua 500 kutoka nchi zote Duniani zikiwemo nchi 33 zinazolima korosho.
Baadhi ya nchi hizo ni pamoja na Ivory Coast, Cambodia, India, Vietnam, Brazil, Indonesia, Sri Lanka, Nigeria, Guinea Bissau, Burkina Faso, Mali, Benin, Ghana, Madagascar, Zambia, Msumbiji, Kenya, Mauritius, Visiwa vya Komoro na wenyeji Tanzania.
Akizungumza na Waandishi wa habari Januari 31, 2025 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Korosho Tanzania , Francis Alfred amesema Mkutano huo unakusudia kutangaza fursa za uwekezaji zilizoko kwenye tasnia ya Korosho kuanzia shambani ambapo wanategemea kupata uwekezaji kwenye mashamba makubwa ya korosho, kuongeza ubanguaji ambapo matarajio ni kuongezeka kwa viwanda vya kubangua na kusindika korosho na bidhaa zake na kuimarika kwa masoko kwa kufungua masoko ya korosho na bidhaa zake ndani na nje ya nchi za Afrika.
"Kwa upekee Mkutano huu utatumika kuhamasisha matumizi ya korosho na bidhaa zake kama vile mafuta ya ganda la korosho (Cashewnut Shell Liquid - CNSL), sharubati (juice), maziwa ya korosho (cashew milk), mvinyo (wine), nyama ya mabibo (cashew apple meat) na pombe kali. Aidha bidhaa nyingine kama ethanol zinaweza kutumika kwenye maabara za hospitali na shule zetu na hivyo kupanua wigo wa soko la korosho". Amesema Alfred.
Amesema mkutano huo utashirikisha wadau mbalimbali kutoka nchi ambazo ni walaji wa korosho ikiwa ni pamoja na Marekani, Nchi za Ulaya, China, Uarabuni, Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini na nchi zingine za bara la Afrika.
Aidha amesema Serikali imefanya juhudi kubwa za kuendeleza zao la korosho ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu sasa imekuwa ikitoa pembejeo za korosho kwa wakulima kwa ruzuku ya 100%.
"Kwa mfano katika msimu wa 2024/2025 ruzuku ya pembejeo ilikuwa shilingi billioni 182. Utoaji wa pembejeo za ruzuku umechagiza kuongezeka kwa uzalishaji kutoka tani 310,000 msimu wa 2023/2024 hadi kufikia tani 410,000 kwa msimu wa 2024/2025 zilizouzwa kupitia minada". Amesema
Pamoja na hayo amesema ukusanyaji wa taarifa za uzalishaji unaendelea kwa kukusanya takwimu za korosho zinazobanguliwa majumbani kwenye vikundi vidogo na watu binafsi pamoja na uzalishaji katika mikoa mipya.
Amesema hadi mwisho wa msimu makadirio ni kuzalisha jumla ya tani 500,000 katika msimu wa 2024/2025.
"Bei ya korosho ghafi katika msimu wa 2024/2025 iliimarika na kufikia shilingi 4,195 kwa kilo ikiwa ni bei ya juu kuliko bei zote zilizopatikana kutoka nchi yetu ipate uhuru.". Ameeleza Alfred.
Hata hivyo amesema pamoja na uwepo wa mahitaji makubwa ya korosho ghafi katika soko la dunia, uamuzi wa Serikali kutumia mfumo wa mauzo wa Soko la Bidhaa (TMX) umesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ushindani katika minada na kuchangia katika kuimarika kwa bei.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ACA, Ernest Mintah amesema Mkutano huo unatarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 400 kutoka nchi mbalimbali duniani ambapo hii itakuwa mara ya tatu kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huukwani mara ya kwanza kwa kipindi cha miaka sita, baada ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo mwaka 2008 na 2019.
Amesema Mkutano wa ACA umekuwa ukijikita kwenye mada kuu inayoundwa kupitia mchakato wa kina ili kuakisi hali halisi na kushughulikia changamoto kuu zinazoikabili sekta ya karanga duniani ambapo katika Mkutano huu itajikita zaidi na kauli mbiu ya "Kufungua Fursa za Uwekezaji katika Karanga kwa Ukuaji Endelevu wa Uchumi."
"Mkutano wa mwaka huu utaangazia hitaji muhimu la kuwekeza kimkakati katika maeneo kama vile utafiti, maendeleo ya uwezo wa binadamu, miongozo ya sera, ubunifu na teknolojia, ufuatiliaji, usalama wa chakula, na mengineyo katika sekta ya karanga ili kuhamasisha ukuaji endelevu". Amesema Mintah.
Nae Mwenyekiti wa Umoja wa wabanguaji wa Korosho, Bahati Mayoma amesema ili kuweza kushiriki kwenye mkutano wa 19 wa mwaka wa ACA kila mshiriki atatakiwa kulipia kiasi cha shilingi 400,000 kwa watakaojisajili na kulipia kabla ya tarehe 15 Oktoba 2025 na shilingi 500,000 kwa watakaojisajili na kulipia baada ya tarehe 15 Oktoba 2025 kwa watanzania .
Aidha kwa wageni amesema itakuwa nia dola za Marekani 500 kwa wanachama wa ACA na dola za Marekani 700 kwa wasio wanachama wa ACA kwa watakaojisajili na na kulipia kabla ya tarehe 13 Agosti 2025 na dola za Marekani 700 kwa wanachama wa ACA na dola za Marekani 1,000 kwa wasio wanachama wa ACA kwa wakakaojisajili na kulipia baada ya tarehe 31 Agosti 2025.
Tanzania Yajivunia Mafanikio Makubwa Katika Sekta ya Utalii
Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii
imevunja rekodi kwa kufikisha watalii milioni 5.3 (5,360,247) ambapo
idadi ya watalii wa kimataifa 2,141,895 na watalii wa ndani 3,218,352
sawa na lengo lililojiwekea la kufikisha watalii milioni 5 ifikapo 2025.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi
Chana (Mb) katika hafla ya kutangaza mafanikio katika sekta ya
utalii,iliyofanyika jijini Dar es salaam, tarehe 31 Januari, 2025.
“Ninatoa
shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maono yake makubwa na uongozi wake
thabiti uliotuwezesha kufikia hatua hii. Kupitia jitihada zake, Tanzania
imepata nafasi kubwa zaidi kwenye ramani ya utalii duniani, na tunazidi
kuona matunda ya kazi hiyo kila siku” amesisitiza Mhe. Chana.
Aidha,
ameweka bayana kuwa bado Wizara yake ina wajibu wa kuifikisha Sekta ya
Utalii katika viwango vya juu zaidi ili kustahimili ushindani katika
soko la Kimataifa na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na wadau
wote wa sekta hiyo kuhakikisha inaendelea kuimarisha huduma, kuboresha
miundombinu, na kupanua masoko ya utalii ili Tanzania izidi kuwa kivutio
kinachopendwa zaidi duniani.
“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, nawapongeza na kuwashukuru wote mliochangia
mafanikio haya. Kazi yenu ni ya thamani kubwa, na tutaendelea kufanya
kazi pamoja ili kuhakikisha mafanikio haya yanazidi kuimarika mwaka hadi
mwaka” amesema Mhe. Chana.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava ameipongeza
Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kuwa na utashi wa kisiasa
katika kuiendeleza Sekta ya Utalii.
"Pamoja na kazi kubwa
mnayoifanya na kufika malengo ya ilani ni jambo kubwa sana lakini bado
tuna kazi ta kufikia malengo kwenye mapato tuko bilioni 4 na malengo ni
bilioni 6" amesema Mhe. Mnzava.
Katibu Mkuu wa Maliasili na
Utalii, Dkt.Hassan Abbasi amesema Wizara imejipanga kimkakati
kuhakikisha kuwa inatimiza lengo la makusanyo ya dola bilioni sita za
kimarekani na kuzidi ifikapo Desemba mwaka huu.
Hafla hiyo
imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maliasili na
Utalii, Taasisi za Serikali, Mashirika binafsi na wadau wa utalii.
Rais Samia Azindua Sera ya Elimu na Kukabidhi Mobile Clinic
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisaini bango maalum lenye ujumbe kuhusu Elimu mara baada ya kukagua mabanda ya maonesho ya masuala ya Elimu katika viwanja vya ukumbi wa mikutano ya Jakaya Kikwete Jijini Dodoma tarehe 01 Februari, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikagua mabanda ya maonesho kuhusu masuala mbalimbali ya Elimu kabla ya kuzindua Sera ya Elimu na Mafunzo kwa mwaka 2014, toleo la 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma tarehe 01 Februari, 2025.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa kampuni ya SC Johnson Family Dkt. Fisk Johnson kutoka Marekani pamoja na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma leo tarehe 1 Februari, 2025.
Matukio mbalimbali wakati wa hafla ya uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo kwa mwaka 2014, toleo la 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma tarehe 01 Februari, 2025.
Matukio mbalimbali wakati wa hafla ya uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo kwa mwaka 2014, toleo la 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma tarehe 01 Februari, 2025.
Dodoma, 1 Februari 2025 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ameshiriki katika hafla muhimu zilizofanyika jijini Dodoma, ikiwa ni hatua nyingine katika kuboresha sekta ya elimu na afya nchini.
Katika tukio la kwanza, Rais Samia amekabidhi magari ya huduma ya afya inayotembea (Mobile Clinic) kwa Wilaya za Sikonge na Uyui, mkoani Tabora. Magari hayo yametolewa na Jakaya Kikwete Foundation kwa ufadhili wa kampuni ya SC Johnson Family ya Marekani.
Hafla hiyo imefanyika Ikulu Chamwino, ambapo Rais Samia amepiga picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa SC Johnson Family, Dkt. Fisk Johnson, pamoja na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Baadaye, katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Rais Samia amezindua rasmi Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 2023.
Kabla ya uzinduzi huo, alitembelea mabanda ya maonesho kuhusu masuala mbalimbali ya elimu na kusaini bango maalum lenye ujumbe kuhusu sekta hiyo.
Hafla hii imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wadau wa elimu na maendeleo, pamoja na wananchi waliojitokeza kushuhudia hatua hii muhimu katika mageuzi ya elimu nchini.
CCM ARUSHA WAUNGA MKONO AZIMIO, RAIS SAMIA NA RAIS MWINYI WAGOMBEA PEKEE 2025
Na Vero Ignatus,Arusha MAELFU ya Wananchi wa Mkoa wa Arusha leo Jumamosi Februari 1, 2025 wamejitokeza kwa wingi kwenye tukio la kuung...
-
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu na timu ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa akiwa katika ...
-
NATIONAL EXAMINATIONS COUNCIL OF TANZANIA PSLE-2014 EXAMINATION RESULTS ARUSHA DAR ES SALAAM DODOMA IRINGA KAGERA KIGOMA ...
-
(Picha na Yahya Charahani) Kwa wale waliokulia maeneo haya, hili ni jambo la kawaida ukitoka mjini, shambani sijui hadi wapi kote ni haya h...