Kamishna wa Nishati na Maendeleo ya Petroli Mhandisi, Hosea Mbise akizungumza katika mkutano wa tatu wa wawekezaji na wadau wa nishati ya umeme ujulikanao kwa jina la Powering Africa uliodhaminiwa na kampuni ya Wind East Africa.
Mkurugenzi na Mwanzilishi wa kampuni ya Six Telecoms Rashid Shamte akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mradi wa umeme wa upepo wa Singida kupitia kampuni ya Wind EA ambao unatarajiwa kuanza uzalishaji rasmi mwishoni mwa mwaka 2017. Shamte alisema hayo wakati wa mkutano wa tatu wa kimataifa wa kuiwezesha Afrika katika utatuzi wa nishati ya umeme umefanyika Dar es Salaam leo. Kulia ni Mkurugenzi wa Mradi huo, Mark Gammons.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa kampuni ya Wind East Africa John Chaggama akifafanua jambo kuhusiana na uwekezaji wao wa Umeme wa Upepo uliopo mkoani Singida. Chaggama alisema mradi huo utatatua tatizo la nishati hiyo hapa nchini mara utakapoanza rasmi uzalishaji mwishoni mwa mwaka 2017.
Wadau na wawekezaji mbali mbali wa nishati ya umeme wakimsikiliza Kamishna wa Nishati na Maendeleo ya Petroli Mhandisi, Hosea Mbise hayupo pichani wakati wa ufunguzi wa mkutano wa tatu wa wawekezaji na wadau wa nishati ya umeme ujulikanao kwa jina la Powering Africa uliodhaminiwa na kampuni ya Wind East Africa.
……………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu
Wakati Serikali ikibainisha kuliondoa Shirika la umeme nchini (Tanesco) katika uzalishaji wa umeme, kampuni ya kuzalisha umeme wa upepo (Wind East Africa) imesema itaanza uzalishaji wa nishati hiyo mwishoni mwa mwaka ujao.
Wakizungumza katika mkutano wa kimataifa wa uwekezaji katika sekta ya umeme, Kamishna wa Nishati na Maendeleo ya Petroli Mhandisi, Hosea Mbise na Mwanzilishi na Mkurugenzi wa wa kampuni ya Wind East Africa, Rashid Shamte walieleza mkakati uliopo katika kuboresha sekta ya umeme nchini ambapo baada ya muda, Tanesco itakuwa na kazi ya usafirishaji tu huku kazi ya uzalishaji ikifanywa na kampuni kama Wind EA.
Mbise alisema kuwa alisema uzalishaji wa umeme unahitaji uwekezaji wa hali ya juu ikiwamo kutoa fursa kwa kampuni mbalimbali kuanza kuzalisha umeme kwa manufaa ya Taifa.
Kwa mujibu wa Mbise, hatua za awali za kuliondoa Shirika hilo la umeme nchini kuwa mzalishaji wa nishati hiyo umeanza na ifikapo 2022, Shirika hilo halitajihusisha na uzalishaji wa umeme zaidi ya kazi ya usafirishaji tu.
“Kwa utaratibu huu, Tanesco sasa itaondoshwa katika mchakato wa kuzalisha umeme na kubaki kuwa msambazaji, hatua tayari zimeanza kwa kuangalia madeni yaliyopo Tanesco na jinsi ya kuyafuta sanjari na kuwachukua watumishi wa Tanesco.
“Ifikapo 2022 hatutakuwa na Tanesco katika uzalishaji wa umeme bali umeme utazalishwa na kampuni mbalimbali na mkakati uliopo ni kwamba hadi kufikia 2030, asilimia 70 ya Watanzania wawe wamefikiwa na huduma ya umeme,” alisema Mbise.
Kwa upande wake, Shamte alieleza kuwa mradi wa umeme wa upepo wa Singida kwa sasa upo katika maandalizi ya kina kuanza na mwaka ujao watakamilisha taratibu mbalimbali kwa mujibu wa sheria za uwekezaji.
Shamte alisema kuwa mradi huo ambao utazalisha 100 Mega Watts mbali ya kutatua tatizo la umeme, utaufanya mkoa wa Singida kubadilika kwa kupata maendeleo makubwa kiuchumi, biashara na hata kijamii.
Alisema kuwa mkataba mikataba ya kumalizia uwekezaji wamradi huo itasainiwa mwanzoni mwa mwezi ujao (Januari 2017).
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa kampuni ya Wind East Africa, John Chagama alisema, mradi wa umeme wa upepo utakapokamilika utawanufaisha Watanzania hasa wakazi wa Singida ambako mradi huo unaanzishwa.
“Kwanza utasaidia kutoa ajira kwa wakazi wa Singida, lakini pia utawanufaisha Watanzania hasa wa kipato cha chini kwani umeme utakuwa wa gharama nafuu,” alisema.
Chagama alisema kuwa umeme wa upepo ni mradi wa kudumu na utawafanya watanzania kupunguza gharama za maisha kwani bei ya umeme itashuka.
No comments:
Post a Comment