Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim Tanzania, Bw. Selemani Ponda, (wa pili kulia) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusiana na uzinduzi wa kituo kipya cha huduma kwa wateja wa benki hiyo kwa njia ya mawasiliano ya simu ikiwa ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo kuboresha huduma zake kupitia teknolojia ya mawasiliano. Pembeni yake ni Mkuu wa Hazina wa Benki hiyo, Bw George Shumbusho (wa pili kushoto), Afisa masoko wa benki hiyo, BwAbdulrahman Nkondo (kushoto) na Meneja Mwandamizi Huduma kwa wateja Bw. Frank Matoro.
BENKI ya Exim Tanzania imezindua kituo chake kipya cha huduma kwa wateja kwa njia ya mawasiliano ya simu ikiwa ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo kuboresha huduma zake kupitia benki hiyo teknolojia ya mawasiliano.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Meneja Mwandamizi Huduma kwa wateja wa Benki hiyo Bw. Frank Matoro alisema pamoja na kusogeza upatikanaji wa huduma kwa wateja wa benki hiyo, vituo hivyo pia vitasaidia kuboresha mahusiano na wateja wa benki hiyo.
“Ni matarajio yetu kwamba wateja wetu watafurahia zaidi huduma bora kutoka kwa wahudumu wenye vigezo na uelewa wa kutosha kuhusiana na masuala ya kibenki kila siku za Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 1:00 jioni na siku za Jumamosi kuanzia saa 2:30 asubuhi hadi saa 7:00 mchana kupitia namba yetu ya 0784 107600,’’ alisema
Kwa mujibu wa Bw Matoro kituo hicho kinatarajiwa kuleta mabadiliko kwenye biashara kupitia huduma za kibenki huku akiongeza: “Ni adhma yetu kuhakikisha kwamba tunapambana siku zote ili tu hali ya kiuchumi kwa wateja wetu iendelee kuwa bora na ni hicho tu ndio kimekuwa kikitusaidia kuwa na matokeo mazuri,’’.
Alibainisha kuwa huduma hiyo ilibuniwa mahususi ili kuleta tija kwa wateja wa benki hiyo kwa kuwa inaenda sambamba na mahitaji yao, mfumo wao wa maisha pamoja na hadhi yao hatua aliyoilezea kuwa itaiongezea benki hiyo uaminifu miongoni mwa wateja wake.
“Pia tunatarajia kwamba huduma hii itatuongezea ukubwa wa soko kwa kuwa itapanua wigo wa kuwafikia wateja, kujiongezea ukuaji wa fursa sambamba na kutoa fursa kwa wateja wetu waweze kutupa mrejesho wa huduma mbalimbali tunazowapatia,’’ alisema.
Akizungumzia hati fungani za benki ya hiyo zinazouzwa katika soko la hisa la Dar es Salaam DSE, Mkuu wa Hazina wa benki hiyo Bw. George Shumbusho alisema idadi kubwa ya watu wameendelea kujitokeza kununua hati hizo huku akibainisha kuwa hati hizo zilizoanzwa kuuzwa tarehe 23 Novemba, 2015 huku zikitarajia kufungwa tarehe 18 Disemba mwaka huu zinalenga kukusanya takribani bilioni 15.
No comments:
Post a Comment