Mratibu wa huduma ya Maji, Afya na Usafi wa mazingira shuleni kutoka wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bi Theresia Kuiwite (Katikati) akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Hedhi Duniani yatakayofanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania tarehe 28 Mei, yatakayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. Kauli mbiu ya mwaka huu Ikiwa “Usisite Kuzungumzia Hedhi”. Wengine kushoto ni Mwandaaji wa maadhimisho hayo kutoka kampuni ya Kasole Secrets LTD, Bi. Hyasintha Ntuyeko na Bi Emmy Manyelezi (Kulia) ambae ni Mratibu wa mradi kutoka shirika la Water Aid Tanzania.
…………………………………………………
Na Mwandishi Wetu,
SERIKALI imetangaza programu maalumu inayolenga kuziwezesha shule za msingi na sekondari hapa nchini kuwa na vyumba maalumu tofauti na choo vitakavyo wawezesha wanafunzi wa kike kupata faragha za usafi wakati wa hedhi wakiwa shuleni.
Hatua hiyo ya serikali iliwekwa bayana na Mratibu wa huduma ya Maji, Afya na Usafi wa mazingira shuleni kutoka wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bi Theresia Kuiwite alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam kuhusu maadhimisho ya siku hedhi duniani yanayotarajiwa kuadhimishwa Mei 28 mwaka huu.
“Lengo ni kupunguza tatizo la mahudhirio hafifu miongoni mwa wanafunzi wa kike ambao wamekuwa wakishindwa kuhudhuria masomo wanapokuwa kwenye hedhi kutokana na ukosefu wa miundombinu rafiki inayoweza kuwapa faragha za wao kufanya usafi wanapokuwa kwenye hali hiyo,’’ alisema.
Kwa mujibu wa Bi. Kuiwite, mpango huo tayari umekwishaanza kutekelezwa katika baadhi ya maeneo hapa nchini ikiwemo wilaya ya Njombe huku akibainisha kuwa kwa sasa wanafunzi wengi wa kike wamekuwa wakishindwa kuhudhuria masomo yao kwa zaidi ya siku 3 hadi 5 kutokana na hedhi jambo linalozorotesha ufahulu wao darasani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Kasole Secrets LTD, Bi. Hyasintha Ntuyeko ambae pia ni mdau na muandaaji wa maadhimisho ya Siku ya Hedhi Duniani alisema Kampuni yake kwa kushirikiana na wadau wengine wameamua kuitumia siku hiyo kuhamasisha mabadiliko ndani ya jamii hususani mila na desturi zinazosababisha suala la hedhi kwa mwanamke lionekane kama ni jambo la aibu kwa jamii.
“Ukweli upo wazi kwamba hata matatizo mengi ya wanawake kuhusiana na uzazi chimbuko lake ni kushindwa kwao kukabiliana na hedhi kwa njia salama haswa walipokuwa katika umri mdogo. Kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ni ‘USISITE KUZUNGUMZIA HEDHI’“, alibainisha.
Kwa mujibu wa Bi. Hyasintha, maadhimisho hayo yataongozwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mhe. Anna Kilango Malecela na yanatarajiwa kupambwa na matembezi ya hiari yatakayoanzia Wizara ya elimu saa 34:00 asubuhi – 06:00 mchana na kumalizikia katika viwanja vya Mnazi Mmoja siku ya tarehe 28,Mei, 2015.
Naye Bi Emmy Manyelezi ambae ni Mratibu wa mradi kutoka shirika la Water Aid Tanzania alitoa wito kwa wadau mbalimbali hususani sekta binafsi kuhakikisha wanaisaidia serikali katika kuhakikisha kuwa vifaa muhimu vinavyohusu masuala ya hedhi zikiwemo pedi za wanawake vinawafikia wananchi wote hususani waliopo vijijini na kwa bei nafuu.
Zaidi ilielezwa kuwa maadhimisho hayo pia yatatoa fursa kwa washiriki kubadilishana elimu juu ya usafi wa hedhi, uzoefu, changamoto na ufumbuzi endelevu kwa ajili ya wasichana wa mashuleni na wanawake kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment