Saturday, May 23, 2015

MIRADI YA UMEME KUFIKIA ASILIMIA 40-45 IKIKAMILIKA KWA WAKATI- SIMBACHAWENE

1
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, (pichani) akisisitiza jambo wakati akizungumza na wananchi wa Vijiji vya Mapanga na Nkome wakati wa ziara yake wilayani Bahi, Mkoani Dodoma. Waziri amefanya ziara Wilayani humo katika vijiji kadhaa kueleza hatua zilizofikiwa katika Utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili, unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika na Umeme Nchini (TANESCO).
2
Meneja wa TANESCO Kanda ya Kati (Dodoma), Mhandisi Deogratius Ndamgoba akiwaeleza wananchi wa Vijiji vya Mapanga na Nkome wilayani Bahi, Mkoani Dodoma, kuhusu kuunganishwa na Huduma ya Umeme kwa vijiji hivyo wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene. Pamoja nae pichani ni Wataalamu kutoka Shirika hilo na nyuma yake ni Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati, Mhandisi Sosthenes Masolla.
3
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Francis Mwonga, akiongea na wananchi wa Kijiji cha Mtitaa wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (katikati). Waziri amefika katika Kijiji hicho kuwaeleza wananchi kuhusu hatua zilizofikiwa za kukiiunganisha Kijiji hicho na Huduma ya Umeme unaotekelezwa na Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili, unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na TNANESCO. Wa kwanza kulia ni Mbunge wa Bahi, Omar Badwel.
4
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene akisalimiana na Wananchi wa Kijiji cha Mtitaa wakati wa ziara yake kijijini hapo.
5
Mbunge wa Jimbo la Bahi, Omar Badwel, akisalimiana na wananchi wa Kijiji cha Kigwe, Wilaya ya Bahi wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene kijiji hapo. Waziri Simbachawene amefika Kijijini hapo ili kueleza wananchi hatua ya Utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili kijijini ulipofikia kijijini hapo.
………………………………………………………………………
Asteria Muhozya, Dodoma
Waziri wa Nishati na Madini George Simbachawene amesema endapo utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini Awamu ya Pili, inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), itakamilika kama ilivyopangwa ifikapo Juni mwaka huu, itawezesha kufikikiwa asilimia 40-45 ya Vijiji na Miji iliyounganishwa na Huduma ya Umeme kwa upande wa Tanzania Bara.
Waziri Simbachawene ameyaeleza hayo wakati wa ziara yake katika Vijiji vya Mtitaa, Nkome, Mapanga, Kigwe na Mpamatwa Wilayani Bahi, Mkoani Dodoma, ambapo amefika katika vijiji hivyo kueleza hatua zilizofikiwa na Mradi huo wa kuviunganisha Vijiji hivyo na Huduma ya Umeme.
“Tangu nchi yetu ipate uhuru, ilikuwa imeunganishwa na huduma ya umeme kwa asilimia 10, uongozi wa Awamu ya Nne ulilenga kufikia asilimia 30, lakini hivi sasa tumevuka na kufikia asilimia 36, haya ni mafanikio makubwa”,amesisitiza Simbachawene.
Aidha, amewataka wananchi wanaopitiwa na Miradi hiyo, kuupokea vizuri uwekezaji huo kwani ni kichocheo kikuu cha uchumi na katika kuboresha maisha yao. “Uwekezaji huu muupokee uboreshe maisha yenu kwani umeme ni ajira, umeme ni maisha bora”,ameongeza Simbachawene.
Katika ziara hiyo, Simbachawene ameambatana na Mbunge wa Bahi, Omar Badwel, Mkuu wa Wilaya ya Bahi Francis Mwonga na wataalamu kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Wataalamu kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...