Mkurugenzi wa Tigo Nyanda za Juu Kusini, Jackson Kiswaga akiwashukuru wananchi wa wilaya ya Iringa baada ya kusimikwa uchifu wa kabila la wahehe.
Mkurugenzi wa Tigo Nyanda za Juu Kusini, Jackson Kiswaga akiwa katika picha ya pamoja na mkuu wa wilaya ya Iringa Angelina Mabula baada ya kusimikwa uchifu wa wahehe.
Mkurugenzi wa Tigo Nyanda za Juu Kusini, Jackson Kiswaga akiwa katika picha ya Pamoja na Waziri wa Ardhi, William Lukuvi, na viongozi wengine wa halmashauri ya wilaya ya Iringa baada ya kusimikwa uchifu wa wahehe.
………………………………………
Na Frank Leonard, Iringa
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Angelina Mabula, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Steven Mhapa na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ni miongozi mwa viongozi mashuhuri waliokuwepo wakati Mkurugenzi wa Kampuni ya Tigo ya Nyanda za Juu Kusini, Jackson Kiswaga akipewa uchifu wa heshima wa kabila la wahehe la mkoani Iringa.
Kiswaga alipewa heshima kutokana na kile kilichoelezwa na wazee wa kabila hilo kwamba wanauona mchango wake mkubwa katika kusaidia maendeleo ya wilaya na mkoa wa Iringa.
Alitawazwa kuwa chifu wa kabila hilo katika hafla iliyohudhuriwa na madiwani mbalimbali wa halmashauri hiyo, wananchi na wageni wengine hivi karibuni katika kijiji cha Mkulula, Iringa Vijijini baada ya kuzindua minara mipya miwili ya mawasiliano katika kijiji hicho na kijiji cha Iguluba.
Wazee na vijana waliokuwepo katika hafla hiyo walisikika wakizungumzia usikivu alionao mkurugenzi huyo wa Tigo katika kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo ya mkoa wa Iringa.
“Mungu ambariki kijana huyu, kwa kweli anafanya kazi inayosaidia kusukuma maendeleo ya mkoa wetu,” alisema mmoja wa wazee aliyejitambulisha kwa jina la Eliasa Mwakayage.
Mwakayage alisema tangu mtandao wa mawasiliano ya simu za mikononi uingie nchini walikuwa wametengwa na teknolojia hiyo mpaka pale kampuni ya Tigo kupitia kwa mkurugenzi huyo iliposikia kilio chao na kuwafikishia huduma hiyo.
Uzinduzi wa minara hiyo iliyohamsha furaha ya aina yake kwa wakazi wa vijiji hivyo ulifanywa kwa pamoja na Lukuvi pamoja na mkurugenzi huyo.
Katika hafla hiyo iliyohuduriwa na wananchi wa vijiji hivyo, madiwani na viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Iringa na Mkoa wa Iringa, Kiswaga alisema minara hiyo mipya imejengwa kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).
“Kukamilika kwa minara hiyo kunatoa nafasi kwa Tigo kutimiza azma yake ya kubadilisha maisha ya watanzania na kuwa ya kidijitali kwa kuwapatia huduma bora na nafuu za mawasiliano kwa kipimo kile kile katika maeneo ya vijijini na mijini,” alisema.
Alisema minara hiyo mipya ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wao wa mwaka huu wa kujenga minara 843 nchi nzima ambayo kati yake 348 inajengwa katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Rukwa na Ruvuma.
Akipongeza jitihada hizo Waziri Lukuvi alisema UCSAF na Tigo wanachangia juhudi za serikali za kuwaingiza wananchi wa vijijini katika dunia ya ustaarabu.
Lukuvi ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Isimani viliko vijiji hivyo alisema; “minara hii itasaidia kuongeza maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa vijiji hivyo na vingine jirani vya kata ya Malengamakali.”
Akionesha furaha yake kwa kupata mawasiliano hayo, mmoja wa wananchi wa kijiji cha Iguluba, Ciprian Mlange alisema; “tulikuwa tunatumia njia za kizamani sana kuwasiliana na ndugu na jamaa na kupata huduma zingine zikiwemo za kutuma na kupokea fedha.”
Mlange alisema mawasiliano hayo yatarahisisha shughuli zao mbalimbali za uzalishaji na biashara kwani watayatumia kufahamu masoko na bei za bidhaa zao bila kusafiri umbali mrefu.
No comments:
Post a Comment