JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
IDARA YA HABARI (MAELEZO)
S.L.P. 8031, Dar es Salaam, Simu:
2110585, 2122771/3, Fax: 2113814, e-mail: maelezopress@yahoo.com
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
SERIKALI YA
TANZANIA NA UNESCO KUADHIMISHA WIKI YA
UKOMBOZI WA BARA LA AFRIKA NA KUZINDUA MRADI WA NYARAKA ZA
URITHI WA TANZANIA
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linalo shughulikia
Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) itaadhimisha Wiki ya Ukombozi wa Bara la
Afrika kuanzia tarehe 25 hadi 29 Mei, 2015 kwa kufanya maonesho ya picha na
kumbukumbu mbalimbali zinazoonesha na kuelezea harakati za ukombozi wa bara la
Afrika pamoja na midahalo mbalimbali itakayowahusisha wasomi na baadhi wa watu
mashuhuri walioshiriki katika harakati za ukombozi.
Maadhimisho hayo yatatanguliwa
na uzinduzi wa Mradi wa Nyaraka za Urithi wa Tanzania (TAHAP)
utakaofanyika tarehe 25 Mei, 2015 katika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa jijini
Dar es salaam. Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa
Mhe. Bernard Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Mradi wa Nyaraka za Urithi wa
Tanzania unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya kwa kushirikiana na UNESCO ukikamilika
unaatarajia kuweka na kutunza kumbukumbu na nyaraka mbalimbali zinazohusu
harakati za ukombozi wa bara la Afrika na ushiriki wa Tanzania kama mwenyekiti
wa iliyokuwa Kamati ya nchi za mstari wa Mbele katika kuzikomboa nchi na
kuvijengea uwezo vyama vya wapigania uhuru kusini mwa bara la Afrika.
Miongoni mwa matukio muhimu katika
maadhimisho hayo ni mdahalo utakaohusu Mchango wa vyama vya Siasa katika
harakati za Ukombozi utakaoongozwa na Mhe. Salim Ahmed Salim na Wazungumzaji
Wakuu watakuwa ni Prof. Issa Shivji na Mhe. Ibrahimu Kaduma, aliyewahi kuwa
Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Mdahalo mwingine Utajikita katika
kuangalia "Mchango wa Wapiganaji/Wanajeshi katika harakati za Ukombozi" tarehe
26 Mei, 2015 utakaofanyika Chuo Kikuu Cha Dar es salaam utakaoongozwa na Prof.
Penina Mlama na Wazungumzaji Wakuu watakuwa Balozi Dkt. Augustine Mahiga
na Brigedia Jenerali Ananias Mwanga.
Tarehe 27 Mei, 2015 kutakuwa na
mdahalo mwingine kuhusu "Mchango wa Wanawake katika harakati za
ukombozi" utakaoongozwa na Prof. Ruth Meena na wazungmzaji wakuu
watakuwa ni Dkt. Alexander Mkulilo na Mhe. Balozi Getrude Mongela (MB). Mdahalo huu
utafanyika katika ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu Cha Dar es salaam.
Mdahalo kuhusu "Mchango wa vyombo vya habari
Wakati wa Harakati za ukombozi" utafanyika Chuo Kikuu Huria Cha
Tanzania tarehe 28 Mei, 2015 na kufuatiwa na mdahalo kuhusu "Mchango
wa Wasanii na Watunzi katika Harakati za Ukombozi" tarehe 29 Mei, 2015
utakaofanyika katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa. Mdahalo huo utaongozwa na Mzee Walter Bgoya. Wazungumzaji
wakuu katika mdahalo huo watakuwa Prof. Penina Mlama na Bw. Zahiri Zahoro.
Maadhimisho hayo yatafungwa Rasmi na
Mhe. Dkt. Fenella
Mukangara, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo tarehe 29 Mei, 2015.
Vyombo vya habari vinaombwa kushiriki kwa kuandika na
kutangaza Matukio hayo muhimu katika kutunza kumbukumbu za ukombozi wa bara la
Afrika katika mikono ya wakoloni na utawala dhalimu wa Afrika Kusini.
MKURUGENZI IDARA YA HABARI
(MAELEZO)
No comments:
Post a Comment