Thursday, May 28, 2015

Diamond Platinumz aibukia programu ya Mziiki


Nyota wa muziki wa bongo flava nchini Diamond Platinumz amewataka wasanii wa Tanzania kusambaza nyimbo zao kwa njia ya teknolojia kama vile Mziiki iliyozinduliwa hivi karibuni ili ziweze kuwafikia watu wengi na kwa wakati huohuo wanamuziki pia kunufaika na jasho lao.

Diamond anasema kuwa  ameamua kazi zake kuziingiza sokoni tofauti na kazi zake za nyuma ambapo baada ya  kushauriana na wadau anaoshirikiana nao kikazi ameamua aingie sokoni kwa njia ya kidigitali kupitia programu ya Mziiki iliyozinduliwa hivi karibuni ambayo pia yeye ni balozi anayeitangaza.

Anasema Tanzania ina wanamuziki wengi wenye vipaji lakini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikiwafanya wasifike mbali zaidi ya muziki wao kusikika hapa nchini na wengi wao kutamba kwa muda mfupi na kupotea katika ulimwengu wa muziki huku wakiwa hawajanufaika na kitu chochote kimaisha na kushauri kuwa  wasibaki nyuma kiteknolojia hasa wakati wa kupeleka kazi zao sokoni iwapo watataka kujikwamua.

“Licha ya kuwepo na changamoto kubwa kama vile kutokuwepo sheria ya hakimiliki inayopelekea wasanii kuibiwa kazi zao na kazi za muziki kutumiwa na vyombo vya habari kama redio na televisheni  bila kuwalipa wahusika chochote. Tatizo lingine linalodumaza muziki wa Tanzania ni uoga wa wanamuziki kubadilika na  kuogopa teknolojia za kisasa kama  hii programu ya kupakua muziki kwenye simu kwa kupitia Mziiki” Alisema.

 Amesema  sababu kubwa iliyopelekea kuamua kufanya biashara ya muziki kupitia progamu hii ni kwamba nyimbo zake ziweze kuwafikia washabiki wake popote na muda wowote kwa urahisi kupitia simu zao za mkononi na anakuwa na uhakika wa kupata mapato tofauti na kama zinavyosambazwa na wasambazaji wa mtaani.

“Duniani kwa sasa hivi kuna ushindani  mkali katika nyanja zote. Sisi kama wanamuziki wa Tanzania tunapaswa kuhakikisha tunatoa muziki wa viwango vya juu na kuhakikisha tunalenga zaidi katika masoko ndani na ya nje kama wenzetu wanavyofanya kusambaza kazi zao kupitia kampuni zinazotumia teknolojia ya kisasa na kumnufaisha msanii kama ilivyo program hii ya Mziiki. Kuna umuhimu mkubwa wa kujiamini, kufanya vizuri ili tuweze kutangaza Tanzania, kutangaza lugha ya Kiswahili na kupata mapato ya kutosha kutokana na kazi ya muziki ambayo ikifanywa kitaalamu inalipa kwa kiasi kikubwa” anasema Diamond Platinumz

Aliwaomba wapenzi wa muziki nchini kuwaunga mkono wanamuziki wa hapa nchini kwa kupakua nyimbo zao kwenye Mziiki  kwa kuwa njia hii iko wazi na inamuwezesha mwanamuziki kujua kirahisi  jinsi kazi zake zinavyokubalika sokoni na inamuwezesha kujua mapato yake tofauti na njia nyingine kama uuzaji wa CD kwenye maduka na mitaani.

Programu ya Mziiki ambayo ilizinduliwa na Vodacom kwa kushirikiana na  Spice VAS Africa  imeanza kufanya kazi na wanamuziki wa hapa nchini na nje ya nchi na katika  kipindi cha muda mfupi tayari imesajili wanamuziki wapatao 1,000  ambao kazi zao  hususani zile mpya zitasambazwa kwa njia ya kidigitali na malengo yake makubwa ni kuhakikisha wanamuziki wanapeleka kazi zao sokoni kwa haraka na kunufaika na jasho lao hususan pale ambapo wananchi wengi watatumia mtandao kwenye simu zao kupakua nyimbo wazipendazo za wanamuziki ambao wamejiunga kwenye tovuti ya kampuni hiyo ambayo inapatikana kwa kubofya tovuti ya www.mziiki.com.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...