Tuesday, February 05, 2008

Kikwete ateua majaji Mahakama ya Rufaa

RAIS Jakaya Kikwete, amewateua majaji wanne wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa majaji wa Mahakama ya Rufani.

Walioteuliwa, ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Dk Steven Bwana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara, Bernard Luanda.

Wengine, ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mohamed Chande Othman na Jaji wa Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara, Dar es Salaam, Sauda Mjasiri.

Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo alieleza katika taarifa yake iliyotangazwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, jijini Das es Salaam jana kuwa uteuzi huo ulianza jana.

"Uteuzi huo umefanyika kwenye Siku ya Sheria Tanzania, siku ambayo huashiria mwanzo wa kalenda ya mwaka wa shughuli za Mahakama nchini," alisema Luhanjo katika taarifa hiyo.

Jaji Bwana ambaye aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu mwaka 1999, pia alipata kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani nchini, Jaji wa Mahakama Kuu ya Visiwa vya Seychelles na Katibu Sheria wa Jaji Mkuu wa Tanzania.

Jaji Luanda alipata kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani nchini na aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania mwaka 2000.

Jaji Mjasiri ambaye alipata kuwa mwanasheria katika Shirika la Sheria Tanzania (TLC) na mwanasheria wa Benki ya Biashara na Maendeleo ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (PTA), aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania mwaka 2002.

Naye Jaji Othman, alipata kuwa mwanasheria katika Chama cha Msalaba Mwekundu (IRC), pia alipata kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Visiwa vya Timor Mashariki na pia kuwa mwendeshaji mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Rwanda (ICTR) mjini Arusha.

Aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania mwaka 2004.

Wakati huo huo, Rais Kikwete amemteua Mohamed Haji Hamza (46) kuwa Balozi na Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, kabla ya uteuzi huo, Hamza alikuwa Kamishna wa Uratibu wa Shughuli za serikali katika Ofisi ya Waziri Kiongozi Zanzibar na uteuzi wake umeanza mara moja.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Hamza anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Ali Shauri Haji ambaye ni Balozi wa Tanzania nchini Misri.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...