Tuesday, June 07, 2016

SERIKALI YATENGA BILIONI 2.7 KUTANGAZA UTALII NDANI NA NJE YA NCHI

SERIKALI kupitia Bodi ya Utalii Nchini (TTB) na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), katika mwaka 2016/17 imetenga kiasi cha Tsh. Bilioni 2.7 kwa ajili ya kuitangaza sekta ya utalii ndani na nje ya nchi.

Akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum (CCM), Maria Kangoye, leo Bungeni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani alisema bajeti hiyo ni ongezeko la asilimia 14.7 za fedha za Serikali zilizotengwa katika bajeti ya mwaka ya 2015/16.

Makani alisema Serikali itaendelea kuboresha sekta ya utalii kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo na vyanzo vingine vya mapato kama ilivyoanishwa katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano 2016/17- 2020/21.

Alisema Serikali pia imepanga kuimarisha Chuo cha Utalii katika kampasi za Bustani iliyopo Dar es Salaam, Temeke na Arusha ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi na umahiri wa wakufunzi, kuboresha upatikanaji wa vifaa vya kufindishia na kuboresha miundombinu ya kampasi hizo.

“Kuhusu uimarishaji wa miundombinu, Wizara yangu imetenga jumla ya Tsh. Milioni 500 katika bajeti ya mwaka 2016/17 ili kukamilisha ujenzi wa jengo la Utalii katika Bustani ya Chuo cha Utalii Tanzania” alisema Mhandisi Makani

Aidha Mhandisi Makani alisema kuwa Chuo cha Utalii Tanzania kwa kushrikiana na Chuo cha Vancouver University cha Canada kupitia mradi wa ISTEP uliopo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Ufundi kitaanzisha mafunzo ya Uongozi katika shahada kuanzia mwezi septemba 2018.

Aidha Mhandisi Makani alisema Serikali inaendelea kuelekeza nguvu katika vyuo vilivyopo kwa kuongeza idadi ya wahitimu wa ngazi ya kati na baadaye wa ngazi ya shahada, ambapo kwa sasa Chuo cha Utalii Tanzania kitaanza kuboresha utoaji wa mafunzo katika tansia za ukarimu na Utalii katika ngazi ya shahada.

No comments:

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR AZINDUA TAWI LA NMB WETE, APOKEA VIFAA TIBA VYA MIL. 12

  NA; MWANDISHI WETU, PEMBA MAKAMU wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Hemedi Suleiman Abdulla, amezindua Taw...