Friday, June 24, 2016

WATUMISHI WA NHIF AMBAO HAWATA BADILI TABIA ZAO KUCHUKULIWA HATUA KALI ZA KINIDHAMU.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga.

Na Mwandishi Wetu.
KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)  amesema atawachukulia  hatua kali za kinidhamu watumishi ambao hawatabadili tabia zao na kuwa chanzo cha malalamiko ya wateja dhidi ya Mfuko.

“Siko tayari kuona wanachama waliotuamini na kutupa michango yao kabla wakitulalamikia kutokana na tabia ya baadhi ya watumishi wachache wanaofanya kazi kwa mazoea... nawapa muda wa wiki mbili kuleta mabadiliko makubwa ya utendaji wa kazi katika maeneo yenu,” aliagiza.

Akizungumza na watumishi wa Mfuko huo katika Ofisi ya Kinondoni, Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bw. Bernard Konga, baada ya ziara ya kustukiza alisema amepata malalamiko kutoka kwa wanachama kuhusiana na utendaji wa ofisi hiyo hususani kuhusu suala la vitambulisho ambapo ameonya tabia hiyo kukoma mara moja.

“Haiwezekani mtu kila siku afuatilie kitambulisho chake... na inapofikia hatua ya mimi kupata malalamiko ina maana suala hili ni kubwa, sasa badilikeni mara moja na tambueni kuwa tuna dhamana kubwa ya kuhudumia afya za Watanzania,” alisema Bw. Konga.

Ziara hiyo aliifanya kwa lengo la kukutana na watumishi ikiwa ni utekelezaji wa maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma ambapo alisema endapo mtumishi ataona hawezi kwenda na kasi iliyopo kwa sasa au kutekeleza majukumu ya Mfuko na maagizo ya Serikali ni vyema akajiondoa mwenyewe haraka kwa kuwa atakuwa kikwazo cha kufikia lengo na matumaini ya Watanzania ya kupata huduma bora kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

Kutokana na hayo, aliwataka watumishi wote kujitathmini, kutoa huduma bora kwa wateja, kuheshimiana na kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake katika maeneo ya kazi ili kuhakikisha wanachama wanapata huduma kwa heshima kubwa.

“Serikali na Watanzania wana matumaini makubwa na Mfuko wetu hivyo kila mmoja aone uzito wa dhamana tuliyopewa na tusiwe chanzo cha kukwamisha matumaini hayo hasa katika kipindi hiki ambacho tunaelekea katika utekelezaji wa mpango wa Afya Bora kwa wote” alisisitiza Bw. Konga.

Aidha, amesema NHIF inakusudia kukutana na watoa huduma ili kujadiliana nao namna bora ya kuboresha huduma zinazotolewa kwa wanachama wa mfuko katika vituo vyao, ikiwemo huduma bora kwa weteja na lugha zinazotumika katika kuwahudumia.

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa sasa una ofisi karibu katika kila Mkoa ambazo lengo lake kuu ni kusogeza huduma kwa wanachama na wananchi kwa ujumla hivyo akatumia mwanya huo kuwataka watumishi wote kujikita katika maadili ya utumishi wa Umma na kutambua unyeti wa sekta wanayohudumia.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...