Wednesday, June 22, 2016

KODI YA USHURU WA BIDHAA KATIKA ADA YA MIAMALA YA UHAWILISHAJI WA FEDHA HAUTAMUATHIRI MTUMIAJI WA MWISHO


Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa za upotoshaji zilizoripotiwa na mitandao ya kijamii kuhusu namna Serikali itakavyotekeleza Bajeti ya mwaka 2016/2017 iliyopitishwa na Bunge jana likiwepo suala la ushuru katika miamala ya kielekrtoniki zitakavyokusanywa bila kuwaathiri watumiaji wa huduma hizo.(Picha Na. Frank Mvungi – MAELEZO – Dodoma) 

Na: Lilian Lundo – MAELEZO - Dodoma

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango amewatoa wasiwasi watanzania juu ya kodi ya ushuru wa bidhaa katika miamala ya benki na simu za mkononi kwamba haitawaathiri wao ila makampuni ya simu.

Mhe. Mpango ameyasema hayo jana  mjini Dodoma alipokuwa akitolea ufafanuzi taarifa za upotoshaji zinazoenezwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu namna Serikali itakavyotekeleza Bajeti ya mwaka 2016/2017 iliyopitiswa jana na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kwa sasa sheria inatamka kwamba ada itatozwa katika kutuma fedha tu, hata hivyo baadhi ya kampuni za simu na benki zimekuwa zikitumia mwanya wa sheria hiyo kupunguza wigo wa kodi kwa kutoza ada wakati wa kupokea,” alisisitiza Mhe. Mpango.

Mhe. Mpango aliendelea kufafanua kuwa, kwa kuwa makampuni ya simu na benki yamekuwa yakitoza ada wakati wa kupokea fedha huku serikali haiwatozi kodi kwa fedha zinazopokewa, hivyo basi Serikali imeamua kutoza ushuru kwenye ada ya kutuma na kupokea fedha au vyote kwa kadri itakavyotozwa.

Aidha Mhe. Mpango alisisitiza kwa kusema kuwa ushuru huo utalipwa na benki na kampuni ya simu na siyo mtumiaji au mpokeaji wa fedha katika miamala itakayofanyika.

Hivyo basi Waziri Mpango ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuhakikisha kwamba tozo hiyo inaendana na uhalisia wa huduma inayotolewa kwa kufanya ukaguzi wa miamala ya makampuni ya simu kabla na baada ya tozo ili yasihamishie mzigo kwa mtumiaji wa mwisho.

Kuhusu suala la kulipa kodi Mhe. Mpango amewasisitiza wananchi kulipa kodi kama inavyotakiwa ili Taifa liweze kujenga uwezo wa kujitegemea na kuwaletea wananchi wake maendeleo ya kweli kwa kuwa hiyo ndio dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...