WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali imedhamiria kuiimarisha Ofisi ya Takwimu ya Taifa ili iweze kutoa huduma bora siyo tu kwa Serikali bali hata kwa wananchi kwa sababu wana haki ya kupatiwa takwimu sahihi.
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Jumatatu, Aprili 27, 2015) wakati akifungua kongamano la siku tatu kuhusu Uongozi na Usimamizi wa Mifumo ya Takwimu liliondaliwa na Taasisi ya Kimataifa ya Takwimu (International Statistical Institute – ISI) kwenye hoteli ya Giraffe jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wakuu wa taasisi za takwimu barani Afrika wanaoshiriki mkutano huo, Waziri Mkuu alisema Kongamano hilo limekusanya washiriki zaidi ya 50 kutoka nchi 31 za Afrika zinazozungumza Kiingereza kwa nia moja ya kuweka msukumo kwenye umuhimu wa matumizi ya takwimu katika kuleta maendeleo ya nchi husika.
“Kama nchi, Tanzania tunakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa takwimu lakini tumeanza kulitazama jambo hili na ndiyo maana nimesema Serikali imedhamiria kuiwezesha taasisi hii ya takwimu ili itoe takwimu sahihi kwa Serikali kwa upande mmoja na kwa wananchi kwa upande mwingine…wao ni wadau wakuu wa takwimu hizi,” alisema Waziri Mkuu.
“Tuna lengo la kuifanya taasisi hii iwe na hadhi ya kimataifa katika kutoa takwimu zake. Sote tunatambua kwamba ulimwengu wa sasa ni wa kidigitali, na bila kuwekeza kwenye hilo hatuwezi kufika mbali,” alisema.
Aliwataka wakuu wa taasisi za takwimu barani Afrika waangalie uwezekano wa kufanya kazi kwa karibu pamoja Halmashauri za miji na wilaya kwani huko ndiko kwenye rasilmali kubwa ya takwimu na ndiko maendeleo ya wananchi yaliko.
“Ukichukua mfano wa Tanzania, tuna Halmashauri za Wilaya na Miji zaidi ya 160. Mkiamua kufanya kazi kwa karibu na Serikali za Mitaa mtapata takwimu za ajabu kwani huko ndiko kwenye miradi yote ya maendeleo. Tukumbuke kuwa asilimia 75 hadi 80 ya Watanzania wote wanaishi vijijini,” alisema.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kufungua kongamano hilo, Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI), Bibi Hawa Ghasia alisema takwimu ni mali ya umma na hazipaswi kutolewa kwa upendeleo.
Waziri Ghasia ambaye alizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Bibi Saada Mkuya, alisema takwimu zenye ubora na ubunifu ni muhimu sana kwa ajili ya kupanga kazi za maendeleo ya Taifa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa, Dk. Albina Chuwa alisema kuna haja ya Serikali za nchi za Afrika kuweka kipaumbele kwenye suala la upatikanaji wa takwimu na lisiwe suala la kuchukuliwa kijuujuu tu, bali lichukuliwe kama sekta kamili ya kipaumbele.
“Naziomba nchi za Afrika zianze kuchukulia takwimu kama sekta ya kipaumbele kwenye mipango yao ya maendeleo ya Taifa… tunapokaribia kuhitimisha muda wa kutekeleza malengo ya milenia (MDGs), tunapaswa kujielekeza kwenye viashiria vipya zaidi ya 300 ambavyo vimeainishwa, hivi viko kwenye ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa”.
“Katika bara la Afrika, kama hatutaamua kuainisha viashiria vyetu wenyewe kuanzia ngazi ya Kitaifa, wataibuka watu na kututengenezea viashiria ambavyo havina uhalisia kwa sababu hawajui matatizo ambayo bara la Afrika linakumbana nayo,” alisema Dk. Chuwa.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
- L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMATATU, APRILI 27, 2015.
No comments:
Post a Comment