Friday, August 29, 2014

MWENYEKITI WA BUNGE MAALUM LA KATIBA, MHE. SAMUEL SITTA AVITAKA VYOMBO VYA HABARI KUANDIKA HABARI BILA KUPOTOSHA UMMA

PIX 7Mjumbe wa Kamati Namba Kumi na Moja, Mhe. Hamad Massauni akiongea na wandishi wa Habari kuhusu kazi na majukumu ya Kamati yake 28 Agosti, 2014.
(Picha zote na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma)

Na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma.
28/08/2014
MWENYEKITI wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta amevitaka vyombo vya habari nchini kuacha uchochezi na chuki wakati vinapohabarisha umma kuhusiana na mchakato wa Katiba Mpya.
Kauli hiyo nimetolewa leo na Mhe. Sitta wakati alipokutana na baadhi ya waandishi wa habari katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma huku akiviasa vyombo vya habari kuachana na kuandika habari zenye kuleta uchochezi na chuki ili kuvuruga mchakato wa Katiba Mpya .
Mhe. Sitta amesema kuwa kuna baadhi ya watu wamekuwa na dhana tofauti kuhusu kazi ifanywayo na Bunge Maalum la Katiba, hivyo ni vema kuepukana nao na kuhabarisha umma taarifa sahihi ili Katiba Mpya iweze kupatikana.
”Kusema tunafanya kazi ya Tume ni upotoshaji mkubwa, sisi tunafanya kazi tuliyotumwa tena kwa uadilifu mkubwa.upotoshwaji mwingine unafanywa na baadhi ya watu ambao hawalitakii mema Taifa letu na hawapendi kuona mchakato wa Bunge la Katiba unaendelea vizuri,” alisema Mhe. Sitta.
Mhe. Sitta ameongeza kwa kutolea ufafanuzi juu ya baadhi ya makundi yaliyowasilisha mapendekezo yao katika Bunge hilo, kwa kusema kuwa maoni yanayoletwa na makundi mbalimbali kwa lengo la kuboresha Rasimu Mpya ya Katiba yanapokelewa lakini sio maoni tu ya mtu binafsi au mwananchi, bali wanapokea maoni kupitia makundi maalum kama yalivyo kwa wafugaji, Wasanii na Wakulima ambao wameshawahi kuwasilisha maoni na mapendekezo yao katika iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba lakini hayakuonekana na mengine yalisahaulika katika Rasimu hiyo.
“Tuna haki na wajibu wa kuyapokea makundi haya ili kutoa Katiba iliyo rafiki kwa wananchi wote,” alisisitiza Mhe. Sitta.
Wakati huohuo, baadhi ya Wenyeviti wa Kamati mbalimbali za Bunge hilo, wamesema wamemaliza kazi ya kuchambua Rasimu hiyo vizuri katika Kamati zao.
Akizungumzia kuhusu kazi hiyo, Mwenyekiti wa Kamati Namba Tatu ya Bunge hilo, Dkt. Francis Michael amesema suala la ardhi lilionekana kuwa nyeti katika Kamati yake.
Dkt. Francis aliongeza kuwa suala la kupokea mapendekezo kutoka kwa makundi mbalimbali si kwamba kila kitu kitawekwa kwenye Katiba Mpya bali ni yale mambo ya msingi.
Naye Mwenyekiti wa Kamati Namba Moja ya Bunge hilo, Mhe. Ummy Mwalimu Ally na Makamu Mwenyekiti wa Kamati Namba Kumi na Moja, Mhe. Hamad Massauni walisema kuwa katika Kamati zao majadiliano yalikwenda vizuri.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...