Aliyekuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993 chini ya mfumo wa vyama vingi, Jaji Lewis Makame amefariki dunia.
Taarifa iliyopatikana jana jioni na kuthibitishwa na mwanaye, Eugene Makame, Jaji Makame alifariki dunia jana mchana katika Hospitali ya AMI Trauma, Masaki Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa takribani mwezi mmoja.
“Nasikitika kuwataarifu ya kwamba mzee (Jaji Makame) hatunaye tena, Bwana ametoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe mbele yake, nyuma yetu, Amen,” alisema Eugene kupitia ujumbe mfupi wa maneno akieleza kuhusu kifo hicho.
Jaji Makame alilazwa katika hospitali hiyo tangu mwishoni mwa Julai, mwaka huu lakini hakukuwa na taarifa rasmi kuhusu kuugua kwake na maradhi yaliyokuwa yakimkabili.
Viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo Rais Jakaya Kikwete walimtembelea hospitalini hapo. Wengine ni Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhan, Jaji Joseph Warioba na Mwenyekiti wa sasa wa NEC, Jaji Damian Lubuva.
Wasifu wake
Jaji Makame aliiongoza NEC tangu mwaka 1993 hadi mkataba wake wa utumishi wa umma ulipofikia ukomo, Julai mwaka 2011.
Aliteuliwa na Rais wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Januari 14, 1993 kushika wadhifa huo na alisimamia uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini, ambao Benjamin Mkapa (CCM) aliwashinda wapinzani wake, Augustine Mrema (TLP) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF).
Pia, ndiye aliyesimamia uchaguzi ambao ulimwingiza madarakani Rais Kikwete mwaka 2005 na 2010.
Kabla ya kuteuliwa kwake kuingia NEC, Jaji Makame alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.
Miongoni mwa makamishna saba wa kwanza wa NEC waliofanya kazi naye ni Jaji Augustino Ramadhan, ambaye pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa NEC, aliyetokea pia Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Jaji Mark Bomani, Solomon Liani, Ben Lobulu, Jaji Julie Manning na Masauni Yussuf Masauni.
Pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Tume za Uchaguzi kwa Nchi Wanachama wa Ushirikiano Kusini mwa Afrika (SADC), Mjumbe wa Taasisi ya Demokrasia Endelevu Afrika, (EISA).
No comments:
Post a Comment