Sheria ya Matumizi ya Fedha katika Uchaguzi sasa kamili

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kesho, Jumatano, Machi 17, 2010, atatia saini Sheria ya Matumizi ya Fedha katika Uchaguzi, katika hafla fupi itakayofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Halfa hiyo fupi itahudhuriwa na viongozi wa taasisi zinazohusiana na masuala ya sheria, utawala bora, mapambano dhidi ya rushwa na michakato ya uchaguzi.

Sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge katika kikao chake kilichopita mwezi uliopita inatekeleza na kuhitimisha ahadi ya Rais Kikwete wakati wa kuzindua Bunge la sasa Desemba 30, 2005, mara baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania.

Rais Kikwete aliliambia Bunge wakati huo kuwa Serikali yake ilikuwa inakusudia kuanza mchakato wa kutungwa kwa sheria ya kihistoria ya kudhibiti matumizi ya fedha katika chaguzi nchini.

Sheria hiyo inalenga kudhibiti matumizi ya fedha na vitendo vya rushwa katika michakato ya uchaguzi ndani ya vyama, na wakati wa uchaguzi wenyewe baina ya vyama, kwa kuwabana watu wanaotaka kupata uongozi kwa nguvu ya pesa.

Sheria hiyo pia itasaidia kuwabana watu wanaogeuza haki yao ya kupiga kura kuwa ni mradi au bidhaa ya kunufaika nayo kipesa kwa kuiuza wakati wa uchaguzi.

Aidha, sheria hiyo inalenga kuleta usawa katika michakato ya uchaguzi baina ya wagombea mbalimbali.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

16 Machi, 2010

Comments

Popular posts from this blog

JESHI LA MAGEREZA NCHINI WAJADILIANA NA NHC NAMNA YA KUENDELEZA MAKAZI MAKAO MAKUU DODOMA

Baraza Jipya la Mawaziri