Jk asaini sheria ya matumizi ya fedha za uchaguzi


RAIS Jakaya Kikwete jana alisaini kwa mbwembwe sheria mpya ya kudhiti matumizi machafu ya fedha kwenye uchaguzi baada ya kualika kwa mara ya kwanza viongozi wa taasisi na vyama mbalimbali kushuhudia tukio hilo.
Lakini viongozi wa vyama vya kisiasa waliopanda kwenye kijukwaa kidogo kumshuhudia rais akisaini sheria hiyo kwa kipindi kisichozidi dakika moja, walionyesha hofu na kuielezea sheria hiyo kuwa ina sura mbili mithili ya sarafu; mmoja ukiwa wa hatari unaoweza kutumika kama kitanzi na upande wa pili mzuri.
Mbali na viongozi hao wa kisiasa, wengine waliofika kwenye viwanja vya Ikulu ni viongozi wa kidini, taasisi za kijamii na sehemu kubwa ya wajumbe wa Baraza la Mawaziri, lakini akakosekana Makamu wa Rais, Dk Mohamed Shein, ambaye yuko mikoani kikazi.
"Sheria nyingine natia saini kimya kimya, lakini hii nitaisaini kwa mbwembwe," alisema Rais Kikwete wakati akifungua mkutano wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) akizungumzia sheria hiyo ambayo aliahidi kuiunda mwaka 2005 baada ya kushinda mbio za urais.
Muda wa kusaini ulipofika, viongozi wa vyama vya siasa walipanda kwenye jukwaa dogo lililoandaliwa kwa ajili ya tukio hilo na baadaye Rais Kikwete aliwafuata na kwenda kukaa kwenye kiti kilichoandaliwa karibu na meza iliyokuwa na kijitabu chenye sheria hiyo.
Katika kile kinachoonekana kuwa alishajua angefanya nini, Rais Kikwete hakuangalia jalada la kijitabu cha sheria hiyo na badala yake alipitiliza kufungua hadi ukurasa wa wenye eneo la kusaini na alipolipata alikiweka mezani na kuanza kusaini.
Picha zinamuonyesha Rais Kikwete akiwa ameuma mdomo wakati akisaini sheria hiyo. Baadaye alisimama na kuwapa mkono viongozi hao wa vyama vya siasa na baadaye kushuka chini ya jukwaa kwa ajili ya picha ya pamoja.
Kikwete alisimama katikati ya viongozi hao, kulia kwake akiwa amesimama Waziri Mkuu Mizengo Pinda, lakini kushoto hakuwepo Dk Shein na badala yake alisimama rais wa Tadea, John Lifa Chipaka akifuatiwa na mbunge wa kuteuliwa, Kingunge Ngombale Mwiru, huku bendi ya polisi ikitumbuiza wimbo wa "Tanzania Nakupenda" na baadaye kufuatiwa na "Tuselebuke" wakati wa vinywaji.
Sheria hiyo ya gharama za uchaguzi imejiwekea rekodi ya kipekee kwa kuwa katika historia ya nchi kwa kuwa haijawahi kutokea rais kusaini sheria hadharani na kufuatiwa na shamra shamra zilizowashirikisha watu wengi mashuhuri.
Hafla hiyo ilikuwa na sura ya sherehe za kitaifa kwa kunogeshwa kwa muziki wa bendi ya polisi na ilitangazwa moja kwa moja na baadhi ya vituo vya redio na televisheni.
Kwenye viwanja hivyo vya Ikulu, yalikuwa yamejengwa majukwaa manne na mojawapo lilikuwa limetengwa kwa kunyanyuliwa juu zaidi ya mengine, maalumu kwa ajili tu ya shughuli hiyo ya utiaji saini na kupigia picha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Philip Marmo ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzungumza katika hafla hiyo na kufuatiwa na Msajili wa Vyma vya Siasa, John Tendwa kuelezea maudhui ya sheria hiyo.
Hafla hiyo imekamilishi ndoto ya Rais Kikwete ya kutunga sheria hiyo ambayo amekuwa akielezea umuhimu wake kila mara katika hotuba zake sambamba na sheria nyingine ya kutenganisha siasa na biashara ambayo muswada wake bado haujawasilishwa bungeni.
Akihutubia taifa mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais Kikwete aliweka wazi kwamba sheria hiyo imetungwa “kwa nia ya kupata majawabu kwa tatizo la matumizi mabaya ya fedha katika shughuli za uchaguzi”.
Licha ya kwamba matukio ya rushwa katika uchaguzi kuwa ni ya muda mrefu, Rais Kikwete alisema yanaimarika siku hadi siku na mbaya zaidi “yanakua kwa kasi ya kutisha na hata kugeuzwa kuwa ndio utaratibu wa kawaida au utamaduni katika chaguzi nchini”.
Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilieleza jana kuwa sheria hiyo ni ya kuwabana wanaotaka uongozi kwa nguvu ya pesa kwa kulenga zaidi kudhibiti matumizi ya fedha na vitendo vya rushwa katika michakato ya uchaguzi ndani ya vyama na wakati wa uchaguzi.
Sheria hiyo inatokana na muswada uliopitishwa na mkutano wa 18 wa Bunge uliomalizika mjini Dodoma Februari 12 na kutafsiriwa na wengi kwamba umelenga kukomesha watu wanaotumia pesa kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM. SOURCE:MWANANCHI

Comments

Popular posts from this blog

JESHI LA MAGEREZA NCHINI WAJADILIANA NA NHC NAMNA YA KUENDELEZA MAKAZI MAKAO MAKUU DODOMA

Baraza Jipya la Mawaziri