Kakobe asalimu amri
Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF),Zacharia Kakobe akizungumza na wanahabari kanisani kwake kuhusu kuridhia kupitishwa kwa nyaya za umeme zenye msongo mkubwa mbele ya eneo la kanisa lake jijini Dar es Salaam jana.Picha na Venance Nestory.
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe sasa amekubali Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupita umeme wa msongo mkubwa mbele ya kanisa lake huku akiendelea kushikilia msimamo kwamba uamuzi uliofanywa na serikali wa kuhalalisha njia hiyo bado siyo sahihi.
Hakuishia hapo bali amekuja na shutma nyingine dhidi ya serikali akisema kwamba shauri hilo limemfumbua macho na kubaini kwamba baadhi ya watendaji wa serikali wana agenda za siri za kuhujumu Ukristo nchini hivyo ameamua kubadili mbinu za mapambano dhidi yao.
Askofu Kakobe aliyasema hayo jana ikiwa ni siku moja baada ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kutoa tamko la serikali la kupuuzia mbali madai ya waumini wa kanisa hilo kwamba kanuni za kitaalamu za kuzuia wasidhurike na njia hiyo ya umeme wa kilovoti 132, haukuzingatiwa.
“Sasa hivi hatuna kipingamizi chochote, waje waendelee na kazi yao,” alisema Kakobe ambaye Desemba mwaka jana alitangaza eneo hilo kuwa ni la hatari kwa wafanyakazi wa Tanesco na tangu wakati huo likawa linalindwa na waumini wa kanisa hilo waliovalia fulana za njano zenye maandishi “Tanesco mwogopeni Mungu.”
Pamoja na kuridhia Tanesco waendelee na mradi huo, Askofu Kakobe alisisitiza kwamba kwenye uamuzi huo haki ilifinyangwa na uamuzi wa kibabe uliochochewa na mambo ya udini, lakini akasema sasa amebadili mbinu na mikakati ya kukabiliana nao.
Akionekana kuzungumza kwa utaratibu na uangalifu mkubwa, alitaja miongoni mwa mbinu zake za sasa kuwa ni kuwasiliana na makanisa mengine ya Kikristo nchini kutaka wajadili hujuma dhidi yao na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.
Miongoni mwa hujuma hizo alidai kwamba ni baadhi ya waumini wa kanisa lake kuanza kubaguliwa kwenye maeneo ya kazi, jambo ambalo alilielezea kuwa “ni la hatari na linaotesha mbegu ya ubaguzi wa udini jambo ambalo ni kinyume na Katiba ya nchi.”
“Hili siyo siri limefanyika. Muumini wetu aliyekuwa anafanya kazi wizara ya nishati aliitwa na kuulizwa anasali wapi na ilipobainika ni muumini wa kanisa hili, kwa muda mfupi tu akakabidhiwa barua ya uhamisho. Huu ni ubaguzi.”
Comments