Mgawo wa umeme wayeyuka




HATIMAYE mgawo wa umeme ambao ulisababishwa na kuharibika kwa mitambo kwenye mabwawa manne, sasa umekwisha baada ya mafundi kufanikiwa kuirekebishwa, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alisema jana.
Ngeleja alisema kuwa kilichokuwa kimetokea ni hitilafu ambayo imeshafanyiwa ukarabati hivyo hali imetengemaa kwa sasa.
“Nadhani Tanesco wameshatolea maelezo hilo... mgao haupo kwa kuwa umeme wa mitambo ya Kihansi na ile nyongeza ya IPTL uko kwenye gridi ya taifa hivi sasa,” alisema Ngeleja.
Waziri Ngeleja alisema hayo jana jijini Dar es Salaam baada ya Makamu wa Rais, Dk Ali Mohammed Shein kuzindua mkutano wa 28 wa sekta ya nishati kwa nchi za kusini mwa bara la Afrika (SAPP).
Ngeleja ametoa kauli hiyo wiki moja baada ya Tanesco kutangaza kuanza kwa mgao kwenye mikoa yote kutokana na kupungua kwa uzalishaji wa umeme kwenye baadhi ya vituo vya uzalishaji.
Mgawo wa umeme umekuwa ukirejea kila mara licha ya Tanesco kutangaza kukomesha tatizo hilo, kutokana na uzalishaji kulingana na mahitaji na hivyo kutokuwa na akiba ya kuweza kuziba upungufu unaosababishwa na kuharibika kwa baadhi ya mitambo.
Tanesco jana walithibitisha kuisha kwa mgao huo na kuwahakikishia wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kwamba wataendelea kupata huduma hiyo bila bughudha.
Meneja uhusiano wa Tanesco, Badra Masoud alisema mafundi wao walikamilisha kazi ya kutengeneza mitambo iliyoharibika juzi jioni.

Alisema mitambo iliyoharibika ilikuwa katika vituo vya Kidatu mkoani Morogoro, Pangani (Tanga), Kihansi (Iringa) na Ubungo jijini Dar es Salaam.
Badra alisema kwa sasa Tanesco wana mkakati wa kumaliza tatizo sugu la upatikanaji wa nishati ya uhakika ifikapo mwaka 2032.
Akizungumzia kuhusu mkakati huo, Ngeleja alisema serikali inatarajia kutumia kiasi cha dola 11 bilioni za Kimarekani katika mpango wa muda mrefu wa kuboresha sekta ya nishati kwa muda wa miaka 25 ijayo.
Alisema kwa mpango wa muda mfupi wa kuanzia 2010-2015 serikali ina mpango wa kutumia kiasi cha dola 2 bilioni za kimarekani kuboresha sekta hiyo.
Kuhusu kupanua na kuboresha miundombinu ya sekta hiyo Ngeleja alisema serikali ina mpango wa kutumia kiasi cha dola za Marekani 7.0bilioni.
“Nishati inayopotea nchini ni asilimia 23 kutokana na miundombinu mibovu, na masuala ya kiutaalamu yamesababisha kuizidiwa kwa gridi ya taifa,” alisema Ngeleja.

SOURCE: MWANANCHI imeandikwa na Boniface Meena Zaina Malongo.

Comments

Popular posts from this blog

JESHI LA MAGEREZA NCHINI WAJADILIANA NA NHC NAMNA YA KUENDELEZA MAKAZI MAKAO MAKUU DODOMA

Baraza Jipya la Mawaziri