Ajali ya Kibamba yaua familia moja
AJALI ya lori na basi dogo iliyotokea juzi Kibamba, Dar es Salaam iliua watu wawili wa familia moja akiwamo mjamzito na kusababisha mtoto mwingine kubaki yatima, imebainika.
Waliokufa ni mjamzito na mumewe ambaye alikuwa akimsindikiza mkewe siku hiyo kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kuhudhuria kliniki.
Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu wa kiume, Issa Ngoro, kaka yake kwa jina la Ibrahim Hussein Ngoro na mkewe Zainab Ali aliyekuwa na ujauzito wa miezi minane ndio waliokumbwa na janga hilo.
Issa alisema kaka yake alikuwa mfanyakazi katika bandari ya Dar es Salaam na alikuwa na kawaida ya kudamka kuwahi kazini akichelea msongamano wa magari barabarani.
“Siku ya tukio, aliondoka alfajiri sana akifuatana na mkewe ili ampeleke kliniki Muhimbili kwanza ili kuwahi foleni ya wajawazito Muhimbili na barabarani na kisha naye awahi kazini kwake,” alisema Issa.
Alisema familia hiyo imeacha mtoto mmoja wa kike, Mwanaidi Ibrahim (4) na mimba aliyokuwa nayo ilikuwa ya uzao wa pili.
Aliongeza kuwa taarifa za ajali hiyo alizipata akiwa msikitini asubuhi, ambapo Imamu aliwatangazia kuwa kuna ajali eneo la darajani na kumlazimu kwenda kushuhudia ingawa hakuwa na uhakika kama alikuwamo ndugu yake.
“Nilipofika pale kwa kweli nilichanganyikiwa kwa jinsi maiti walivyokuwa wamekatikakatika na baada ya kuona mjamzito akitolewa, ndipo nikamwaza shemeji yangu, na baadaye kidogo nikaona mguu wa kaka ukitolewa na niliutambua kwa kuwa ulikuwa na kovu kwa nyuma,” alisema Issa.
Issa aliongeza kuwa baada ya hapo, alimpigia kaka yake simu ambayo ilikuwa haipatikani, na baadaye ikambidi arudi nyumbani huku akiogopa kumwambia mama yao na walipopiga simu ya shemeji yake ikapokewa na polisi na kuarifiwa kuwa anayepigiwa amekufa na yuko mochari.
Alisema siku moja kabla ya tukio, alikutana na kaka yake akitokea kwenye shughuli zake na alimsisitiza kukazania elimu kwa kuwa wakati mwingine alikuwa akimchangia ada na nauli ya shule.
Mdogo wa marehemu Zainab, Sharifa Ali, alisema siku moja kabla ya tukio, dada yake alimpigia simu akimweleza kuwa angekwenda kliniki na baada ya hapo angepitia kwa bibi yao Magomeni.
Alisema dada yake hakuwa na uchungu wa kujifungua na kwamba alikuwa akienda kwa ratiba za kawaida. Wawili hao walizikwa jana katika eneo hilo, katika makaburi matatu tofauti.
Katika hatua nyingine, eneo la Kibamba taarifa kuu iliyotawala midomoni mwa wakazi ilikuwa msiba huo ambapo asilimia kubwa ilikuwa ya wakazi wa pale, hali iliyowafanya kutafakari wahudhurie msiba upi.
Ajali hiyo ilisababisha vifo vya abiria wote 11 waliokuwa katika Toyota Hiace namba T615 AJW ikitokea Kibamba kwenda Ubungo ambapo iligongana na lori la mafuta ya taa aina ya IVECO Fiat namba T189 ABP na tela lake namba T192 ABP.
Hadi jana asubuhi watu watano walishatambuliwa.Imeandikwa na Lucy Lyatuu; SOURCE:HABARI LEO
Comments