Marekani yatoa Sh647.4 milioni BoT
SERIKALI ya Marekani imeipa Benki Kuu ya Tanzania(BoT), dola 498,000 za Kimarekani (sawa na Sh647.4 milioni za Kitanzania) kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya mawasiliano na teknolojia.
Fedha hizo zimetolewa na Wakala wa Biashara na Maendeleo wa Marekani (USTDA), ambayo umekuwa ikisadia nchi zinazoendelea na zenye kipato cha kati, katika masuala kama ya utafiti, mafunzo ya kibiashara na kutoa elimu ya kuwezesha kumudu miundombinu ya kisasa katika kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara.
Kutokana na umuhimu wa miundombinu ya teknolojia ya mawasiliano ya BoT, fedha hizo zitasaidia kupitia upya mfumo uliopo, sera iliyopo ya usalama, namna ya kuzifuatilia na kuzikomboa fedha zilizopotea kutokana na majanga na mipango ya maendeleo ya biashara.
Msaada huo pia utasaidia kuboresha mapitio ya kazi za kila siku za BoT.
Makubaliano ya kutolewa kwa fedha hizo yalifikiwa jana kati ya gavana wa BoT, Benno Ndulu na balozi wa Marekani nchini, Alfonso E. Lenhardt ambaye alisema fedha hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa teknolojia ya mawasiliano ya benki hiyo.
“Msaada huu utasaidia juhudi za BoT kujiwezesha kimawasiliano na katika shughuli zake za kila siku; kuwa na uwazi pamoja na mpangilio mzuri wa bajeti,” alieleza Lenhardt.
SOURCE: UBALOZI WA MAREKANI
Comments