Rais apokea ripoti ya CAG




RAIS Jakaya Kikwete amepokea ripoti za Ukaguzi wa Matumizi ya Fedha za Serikali na Taasisi zake za mwaka 2008/2009 kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Ludovick Utouh.

Ripoti alizopokea Rais ni za Ukaguzi wa Taarifa za Fedha ambazo zinahusu Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na za Mashirika ya Umma.

Ripoti zingine ni za Ufanisi ambazo ni ripoti ya jumla ya Ukaguzi wa Ufanisi, ukaguzi wa ufanisi na thamani ya Fedha kwenye sekta ya ujenzi wa Barabara.

Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, iliyorekebishwa mwaka 2005, pamoja na sheria ya Ukaguzi wa Umma ya mwaka 2008 na Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa ya mwaka 1982 iliyorekebishwa mwaka 2000, mara baada ya kupokea ripoti hiyo anatakiwa kumwagiza Waziri mwenye mamlaka husika kuziwasilisha ripoti hizo Bungeni.

Katika mazungumzo hayo Utouh amemueleza Rais Kikwete juu ya mafanikio mbalimbali ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kutoka mwaka 2005/2006 hadi za 2008/2009 na kuonyesha kuridhishwa nazo.

Baadhi ya mafanikio hayo ni uwezo wa ofisi yake kuwakilisha ripoti nne kwa mwaka huu 2008/2009 kutoka ripoti mbili mwaka uliopita wa 2005/2006.

Itakumbukwa kuwa Ripoti za mwaka 2005/2006 zilijadiiwa chini ya Uenyekiti wa Rais Kikwete katika vikao muhimu vitatu ambacho ni kikao cha Baraza la Mawaziri, Kikao cha viongozi wakuu wa Serikali Kuu kilichofanyika na kikao cha Viongozi Wakuu wa Serikali za Mitaa vyote vilifanyika Aprili , 2007.

Bwana Utouh pia ameeleza kuwa tofauti na ripoti za mwaka 2005/2006 ambazo uandaaji wa taarifa za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa ulitumia viwango na miongozo ya ndani ya nchi, uandaaji wa ripoti hizi mpya umetumia viwango vya kihasibu vya Kimataifa.

Hatua nyingine kubwa iliyofikiwa na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ni kuwa ukaguzi wa Balozi za Tanzania za ripoti iliyopita ulifanyika kwa kutumia sampuli chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wakati ripoti hii ya leo ukaguzi umefanyika kwa Balozi zote na kila Balozi kupewa hati yake ya Ukaguzi na katika ukaguzi mzima hati za mwaka huu zinaonyesha kuboreka zaidi kuliko za kipindi kilichopita.

Akipokea Ripoti hizo Rais Kikwete aliishukuru ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kazi hiyo na kuahidi kuijengea ofisi hiyo ili ifanye kazi vizuri zaidi.

“ Tutafanya jitihada ya kuwawezesha zaidi, ni muhimu kuongeza watumishi, mishahara, vitendea kazi ili mfanye kazi vizuri zaidi”.

Alisema Rais na kusisitiza kuwa nidhamu kwenye matumizi ya fedha ni muhimu na kwamba tangu serikali ilipoelezea na kukuza uelewa na umuhimu wa nidhamu katika matumizi ya fedha kwa viongozi na watendaji, nidhamu imeanza kuonekana na hivyo hakuna budi kujenga nidhamu zaidi.

Comments

Popular posts from this blog

JESHI LA MAGEREZA NCHINI WAJADILIANA NA NHC NAMNA YA KUENDELEZA MAKAZI MAKAO MAKUU DODOMA

Baraza Jipya la Mawaziri