Thursday, July 24, 2008

TID afungwa jela mwaka mmoja


Picha juu msaniii TID akitoka kwenye Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam Muda Mfupi baada ya kuhukumiwa kifungo cha Mwaka Mmoja Leo..
-----------
MAHAKAMA ya Wilaya ya Kinondoni imemhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela msanii wa muziki wa kizazi kipya,Bongo Fleva,Khalid Mohammed 'TID' baada ya kutiwa hatiani kwa kujeruhi. TID,26,mkazi wa Kinondoni Hananasif,Dar es Salaam alitiwa hatiani jana katika mahakama hiyo iliyokuwa imefurika watu mbalimbali,wakiwamo ndugu wa msanii huyo, wazazi na baadhi ya marafiki zake,wote wakitaka kujua hatima ya msanii huyo.

Hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo,Hamisa Kalombola kabla ya kutoa hukumu hiyo alisema kwamba kesi hiyo,kwa upande wa mlalalamikaji ilikuwa na mashahidi wanne na ushahidi waliota mahakamani, umeonyesha wazi kuwa msanii huyo alitenda kosa hilo.

Hakimu Kalombola aliendelea kusema kuwa,kulingana naushahidi uliotolewa umeonyesha wazi mtuhumiwa alitenda kosa kwa makusudi,hivyo kuishawishi mahakama kumtia hatiani.
Kwa upande wa mshtakiwa hakuwa na shahidi,kwani shahidi aliyepaswa kutoa ushahidi alielezwa kuwa alikuwa ni rafiki yake wa kike ambaye alikuwepo katika tukio,lakini ilielezwa mahakamani hapo kuwa alikuwa safari na hivyo kumsababisha rafikie kukosa shahidi.

Kabla ya kutoa hukumu,mahakamani hapo,Hakimu Kalombola alisoma maelezo ya awali ambako ilidaiwa kuwa Julai 2 mwaka jana saa 6:30 usiku katika Hoteli ya Slipway,eneo la Masaki wakiwa katika ukumbi wa burudani,mtuhumiwa alimpiga mlalamikaji Ben Mashibe kwa kutumia trei la chupa za bia na kumsababishia maumivu makali.
Ilidaiwa kuwa kitu kilichomsabisha msanii huyo kuanzisha fujo ni kutokana na begi alilokuwa ameshika rafiki wake huyo wa kike,kutoonekana kwa muda huo,hivyo kusababisha watu waliokuwapo mahali pale ikiwa ni pamoja na mlalamikaji kuanza kushambuliwa.
Baada ya kusoma maelezo,Hakimu alimpa nafasi mtuhumiwa kujitetea,ambako alisema kwamba alikuwa amepitiwa siku ya tukio kutokana na pombe alizokuwa amekunywa,hivyo akaiomba mahakama iahirishe kutoa hukumu hiyo.

Mtuhumiwa alijitetea kuwa anayo familia inayomtegemea katika kuwalea, isitoshe mama yake mzazi hana kazi, naye pia anamtegemea kwa kila kitu.Kwa upande wake,Mwendesha Mashtaka, Inspekta wa Polisi,Benedict Nyagabona alidai kuwa kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani umeithibitishia kuwa mtuhumiwa alitenda kosa,hivyo anastahili adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine.

Inspekta Nyagabona alidai kuwa kuwa kitendo cha mtuhumiwa kunywa pombe kupita kiasi hadi kuwasababishia watu madhara,ni kinyume na sheria,hivyo anatakiwa apewe adhabu kali kwa kuvunja sheria na pia kuleta madhara kwa jamii.Hata hivyo,wakati akiondolewa mahakamani hapo,msanii huyo alionyesha dhahiri uso wa majonzi huku ndugu zake nao wakionyesha kufadhaika.

Kabla ya kupanda karandinga,TID alikabidhi mali zake ikiwamo simu ya mkononi kwa mtu ambaye alidaiwa ni msanii mwenzake,ambaye hata hivyo alisikika akimweleza asikate tamaa ya maisha,ataweza kumaliza kifungo chake.Habari hii kwa msaada wa Elizabeth Suleyman.Picha na Mdau Msimbe.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...