Tuesday, July 22, 2008
Mizengwe dhidi ya Dk Masau
MWANZILISHI na Rais wa Hospitali ya Taaisi ya Moyo Nchini (THI) Dk Ferdinand Masau amegoma kuhama katika jengo la Shirika la Taifa ya Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambako anaendesha shughuli zake.
Dk Masau alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa mkutano wa VC uliopo ndani ya Jengo la Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) muda mfupi baada ya kumalizika kwa semina ya madaktari wa moyo.
Dk Masau alisema hawezi kuhama katika jengo hilo kwa sababu NSSF imeshindwa kutimiza makubaliano yao wakati walipompangisha na kwamba kuna wagonjwa pamoja na mali za THI.
“Kwanza siwezi kuhama katika jengo hilo kwasababu kuna wagonjwa 15 wamelazwa ambapo kati yao wagonjwa 5 wanategemea kufanyiwa upasuaji wa moyo wakati wowote, pili vitu ambavyo viko ndani ya jengo hilo ni zaidi ya bilioni, makubaliano yetu ilikuwa ni kutengeneza jengo hilo ili liwe na hadhi ya hospitali ya moyo kitu ambacho walishindwa kuyatimiza ,”alisema Dk Masau.
Alisema moja ya makubaliano yao ni kwamba NSSF wamtengenezee jengo liwe na hadhi ya Hospitali ya Moyo.
Alisema baada ya makubaliano hayo NSSF walimpelekea taarifa kuwa kazi hiyo imeshamalizika hivyo anachotakiwa kufanya ni kukubali kusaini mkataba wa kulipangisha jengo hilo.
“Nilikubali kusaini mkataba wa kama mpangaji baada ya NSSF kunihakikishia kuwa wamenitengenezea jengo hilo kama nilivyowaeleza, lakini baada ya kusaini mkataba na kuingia ndani ya jengo nikagundua kuwa kuna baadhi ya maeneo hayajatengenezwa kama nilivyoyahitaji,”alisema Masau na kuongeza:
“Baada ya kubaini mapungufu hayo tulikubaliana niendelee kulitumia jengo hilo wakati marekebisho hayo yanafanyika, lakini hayo hayakufanyika badala yake nilishangaa kuona taarifa ya kuitwa mahakamani kwa kesi ya madai miezi miwili baada ya mkataba huyo,”alisema.
Alifafanua kuwa baada ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa mahakamani miezi miwili baadaye hukumu ilitolewa na mahakama ikaamuru aondolewe katika jengo hilo na kwama baada ya amri hiyo alimfuata Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambapo Waziri aliwataka wayamalize nje ya mahakama chini ya Wizara ya Kazi Ajira na Maendeleo ya Vijana.
Uamuzi wa kumuondoa katika jengo hilo lilitolewa jana na Shirika hilo katika vyombo vya habari iliyokuwa na kichwa cha habari ilisomeka kama taarifa kwa umma akidaiwa kushindwa kulipa deni la jengo hilo lenye thamani ya Sh 2.3 bilioni.
Sehemu ya taarifa hiyo ilisema kuwa NSSF inatoa taarifa kwa wananchi wote kuwa, kwa muujibu wa amri ya Mahakama Kuu (kitengo cha Ardhi) iliyotolewa Septemba 11 mwaka jana katika shauri na 158/2007 kati ya NSSF na Taasisi ya moyo Tanzania.
“NSSF itatwaa jengo lake lililojulikana kama”Hosteli ya Tazara” ambapo kwa sasa limepangishwa na THI Julai 25 mwaka huu hivyo wagonjwa wote na familia zao wanashauriwa kufanya mpango mbadala ya hospitali ya kuhama au kuhamisha wagonjwa wao kabla ya tarehe hiyo kufika,”ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Hata hivyo, kufuatia taarifa za ndani ya NSSF zilizonaswa na Mwananchi zimebaini serikali ilishawahi kutoa tamko kuwa haiwezi kingilia zaidi mgogoro huo na kuwataka wamalize mgogoro huo kwa mujibu wa maamuzi ya mahakama.
Kwa mujibu wa nyaraka hizo za siri pia ilibaini kuwa Julai 5, Waziri wa Kazi Ajiri na Maendeleo ya Vijana Profesa Juma Kapuya alimuandikia Dk Masau barua iliyosema kuwa endapo atashindwa kulipa sehemu ya deni hilo kama walivyokubaliana katika kikao cha Julai Mosi mwaka huu NSSF itaendelea na uamuzi wake wa kumtoa ndani ya jengo hilo.
“Tulikubaliana kuwa endapo taasisi yako itashindwa kulipa sehemu ya deni hilo kama inavyopendekezwa basi NSSF itaendelea na uamuzi wake wa kuitoa hiyo THI kwenye jengo hilo kama iliyoamuriwa na mahakama bila kutoa notisi nyingine,”ilisema sehemu ya barua hiyo ya Waziri Kapuya.
Hata hivyo, nakala ya barua ilipelekwa kwa Waziri Mkuu,Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii na NSSF. Habari na Jackson Odoyo na Saida Amini
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA
Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...
-
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu na timu ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa akiwa katika ...
-
NATIONAL EXAMINATIONS COUNCIL OF TANZANIA PSLE-2014 EXAMINATION RESULTS ARUSHA DAR ES SALAAM DODOMA IRINGA KAGERA KIGOMA ...
-
Adam Malima James Wanyancha Hamis Kagasheki RAIS Jakaya Kikwete ameteua Baraza la Mawaziri, huku likiwa na sura na damu mchanganyiko. Bar...
No comments:
Post a Comment