Wednesday, January 20, 2016

WAZIRI MBARAWA AITAKA TTCL KUFANYA BIASHARA YA UHAKIKA

Y1
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akiweka saini kwenye kitabu cha kumbukumbu mara alipowasili Mkoani Mtwara kwa Ziara ya Kukagua miradi inayotekelezwa na Wizara hiyo, kulia ni Mkuu Mkoa wa Mtwara Bi. Halima Dendegu na kushoto ni Katibu Mkuu sehemu ya Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora.
Y2
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,Profesa Makame Mbarawa akikagua Mitambo ya Mawasiliano ya TTCL Mkoani Mtwara kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Dkt.Kamugisha Kazaura na wadau wengine wa mawasiliano.
Y3
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akisikiliza taarifa ya utekelezaji wa vivuko cha Mv. Mafanikio na Mv. Kilambo vinavyotoa huduma kati ya Msangamkuu – Msemo na Kilambo –Msumbiji kutoka kwa Kaimu meneja wa TEMESA mkoa wa Mtwara Bi. Engeltraud Mbemba.
Y4
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akizungumza na baadhi ya abiria wanaotumia kivuko cha Mv. Mafanikio kabala ya kuanza kwa safari kutoka Msangamkuu kwenda Msemo.
Y5
Mkuu wa bandari ya Mtwara Bw. Ogullo Peter akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa katika kikao kati ya Waziri huyo na wafanyakazi wa bandari Mtwara.
Y6
Captain Mkuu wa bandari ya Mtwara Hussein Bakari Kasuguru akimueleza jambo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kulia ni Mkuu wa Wilaya Mtwara Bi. Fatma Salum Ally.
Y7
Mkuu wa bandari ya Mtwara Hussein Bakari Kasuguru (Kushoto), akipokea maelekezo kutoka kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kulia ni Mkuu wa Wilaya Mtwara Bi. Fatma Salum Ally.
Y8
Mojawapo ya Meli kubwa zinazotia nanga katika bandari ya Mtwara ikiwa tayari kwa kupakua mzigo.
………………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ameitaka kampuni ya simu ya TTCL kutumia vizuri mkongo wa taifa kufanya biashara ili kuiwezesha kushindana katika soko na kuiongezea Serikali mapato.
Akizungumza mara baada ya kukagua mitambo ya TTCL mkoani Mtwara Prof. Mbarawa amesema kwa kuwa kampuni hiyo sasa ni ya Serikali kwa asilimia mia moja inatakiwa kufanya biashara kwa kuongeza wateja wapya na kuhakikisha inapata fedha nyingi zitakazotokana na wateja wengi kuunganishwa.
“Hakikisheni mnaunganisha wateja wakubwa katika mkongo wa taifa wa mawasiliano kama vile Benki, Viwanda, Mifuko ya Hifadhi Jamii na vyombo vya habari ili huduma ya mawasiliano hapa Mtwara na kwingineko nchini iwe ya uhakika na hivyo kukuza uchumi wenu binafsi na Taifa”, amesema Prof. Mbarawa.
Kwa sasa Kampuni ya TTCL inamilikiwa na Serikali kwa asilimia Mia moja baada ya kuilipa kampuni ya BAT Airtel shilingi Bilioni 14.9 kuondoa ubia uliokuwepo hapo awali ambapo kampuni hiyo ilikuwa ikimilikiwa na Serikali kwa asilimia 65 na Bat Airtel kwa asilimia 35.
Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Dkt. Kamugisha Kazaura amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa kampuni hiyo imejipanga kutumia fursa ya mkongo wa taifa wa mawasiliano kufanya biashara nchini kote na kuongeza gawio kwa Serikali.
Katika hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amekagua Bandari ya Mtwara na kuwataka viongozi na wafanyakazi wa bandari hiyo kufanya kazi kwa ubunifu ili kuvutia wafanyabiashara kutumia bandari hiyo na kuhakikisha meli zinazoshusha bidhaa hapo zinahudumiwa kwa wakati.
Ametaka Wafanyakazi wa bandari kuwa waadilifu na wawazi ili kazi yao kuwa kwa manufaa ya taifa na sio binafsi ili kujenga taswira nzuri kwa jamii hapa nchini.
“Nawahakikishia hatutamuonea mtu wala hatutamwachia mtu mbadhirifu kutia hasara taasisi hii muhimu kwa nchi tunafanya hivyo ili kutenda haki kwa watanzania wote”, amesistiza Prof. Mbarawa.
Ameitaka Mamlaka ya Bandari kukusanya shilingi trilioni moja kwa mwaka mpya wa fedha kutoka bilioni 600 ilizokuwa ikikusanya mwaka huu na kusisitiza umuhimu wa kutenda kazi kwa ubunifu na weledi.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Bandari Mkoani Mtwara (Dowota) Bw.Abilahi Darusi amemueleza Waziri Mbarawa kuwa kwasasa wafanyakazi wengi wa bandari wanafanya kazi kwa hofu hivyo ni vyema Waziri akakutana na makundi ya wafanyakazi ili kuelezwa hali halisi ya Bandari nchini.
Naye Capten Mkuu wa Bandari Mtwara Hussein Bakari Kasuguru amemueleza Waziri Prof. Mbarawa kuwa kwa sasa meli zinazotia nanga katika bandari ya Mtwara ni kubwa hivyo aangalie umuhimu wa kujengwa eneo kubwa la kuegeshea Meli hizo ili kuendana na mahitaji ya sasa.
Bandari ya Mtwara inayohudumia Lindi na Zanzibar ilijengwa mwaka 1950 na ina gati lenye ukubwa wa mita 385 na kina cha mita 9.8 na inahudumia tani zaidi ya laki mbili na mia tano sabini na sita kwa mwaka.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...