Saturday, January 16, 2016

SERIKALI YAOKOA ZAIDI YA BILIONI 3 KWA KUDHIBITI UTOROSHAJI NA BIASHARA HARAMU YA MADINI NCHINI

bffdGeita-gold-mineMoja ya majukumu ya Wakala wa Ukaguzi wa madini Tanzania (TMAA) ni kufuatilia na kuzuia utoroshaji/magendo na biashara ya madini unaopelekea ukwepaji wa ulipaji mrabaha kwa kushirikiana na taasisi nyingine husika za Serikali zikiwemo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Idara ya Uhamiaji.
Taarifa za matukio ya udhibiti wa utoroshaji na biashara haramu ya madini zilizopo zinaonesha kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai 2015 mpaka Januari 13, 2016 kulikuwepo na jumla ya matukio 14 ya utoroshaji wa madini ambapo madini yenye thamani ya Dola za Marekani 1,474,194 milioni (zaidi ya Shilingi bilioni 3,235,856,181) yalikamatwa na wakaguzi wa Wakala kupitia Madawati ya Ukaguzi yaliyopo katika viwanja vya ndege vya Dar es Salaam (JNIA), Kilimanjaro (KIA) na Mwanza.
Katika matukio ya hivi karibuni ya ukamataji wa madini katika viwanja vya ndege, madini yenye thamani ya jumla ya Shilingi milioni 11,217,300 yalikamatwa na wakaguzi wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola.
Raia mmoja wa kigeni na mwingine wa Tanzania walikamatwa wakiwa na madini hayo bila kuwa na kibali chochote cha usafirishaji kulingana na Sheria ya Madini ya mwaka 2010. Raia wa kigeni (jina limehifadhiwa) ambaye alikuwa anasafiri kwenda Bangkok alikamatwa akiwa na madini aina mbalimbali ikiwemo almasi, aquamarine, sapphire, green tourmaline, quartz na rhodolite.
Tukio la pili, mtuhumiwa mwingine ambaye ni raia wa Tanzania aliyekuwa akisafiri kwenda Ujerumani alikamatwa akiwa na madini mbalimbali ikiwemo amethyst, moonstone cabochon, rulilated quartz (cabochon), rulilated quartz(faceted), chrysoprase, green tourmaline, ruby, red garnet, green quartz, zircon na rhodolite.
Kufuatia Matukio hayo wahusika wote wamechukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kufunguliwa kesi mahakamani.
Wakala unatoa rai kwa Umma kujiepusha na shughuli za utoroshaji/magendo na biashara haramu ya madini, kwani hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa yeyote atakayebainika/kukamatwa akijihusisha na shughuli hizo. Aidha, madini yatakayokamatwa yakisafirishwa kinyume cha sheria na taratibu zilizopo yatatafishwa na Serikali.
Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini inatoa wito kwa yeyote atakayetoa taarifa za utoroshaji/magendo na biashara haramu ya madini kwa Kamishna wa Madini au Wakala ambazo zitawezesha ukamataji wa madini, atazawadiwa fedha taslimu ambazo ni sawa na asilimia 5 ya thamani ya madini yatakayokamatwa na kunadiwa. Kwa mawasiliano ya haraka, wananchi watumie barua pepe info@tmaa.go.tz na simu 022-2137142 au 022-2601819.
IMETOLEWA NA
DOMINIC RWEKAZA
MTENDAJI MKUU
WAKALA WA UKAGUZI WA MADINI TANZANIA
15 JANUARI, 2016

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...