Thursday, January 14, 2016

MKUTANO WA SSRA WAFANYIKA MKOANI IRINGA

RR1
Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya jamii, Sabato Kasuri akifafanua majukumu ya mamlaka hiyo kwa watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa wakati wakitoa dukuduku lao kuhusu mifuko ya hifadhi ya jamii.
RR2RR3
Baadhi ya watumishi katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa na idara zake wakifuatilia mjadala kuhusu mifuko ya hifadhi ya jamii ulioendeshwa na mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) mjini Iringa jana.
…………………………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu, Iringa
WATUMISHI wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa na idara zake wameishtaki kwa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) baadhi ya mifuko ya hifadhi ya jamii wakiilalamikia kwa mambo makubwa matano ikiwemo ucheleweshaji wa mafao kwa wanachama wake wastaafu.
Katika kikao kilichofanyika juzi mjini hapa baina ya SSRA na watumishi hao; watumishi hao walisema uzoefu toka kwa baadhi ya wastaafu wengi unaonesha kwamba inawachukua muda mrefu kupata mafao yao.
Afisa Utumishi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa, Gasto Andongwisye alitoa mfano akisema; “baadhi ya watumishi waliostaafu kabla ya mwezi Julai mwaka jana hawajapata mafao yao hadi leo na imekuwa ni kilio kikubwa ofisini kwangu.”
Akijibu lalamiko hilo, Afisa Uhusiano wa SSRA, Sabato Kasuri alisema ucheleweshaji wa mafao ni changamoto ambayo tayari imefanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa baada ya kubainika ilikuwa ikisababishwa na na ukosefu wa kumbukumbu sahihi za walengwa.
Alisema mamlaka yao imetoa miongozo mbalimbali ya kuboresha sekta ya hifadhi ya jamii na katika suala la kumbukumbu kuna miongozo ya utunzaji wa kumbukumbu na takwimu ambayo kama ikitumiwa ipasavyo hakuna mstaafu atakayecheleweshewa mafao yake kwasababu zilizondani ya uwezo wa mifuko.
Ili kuondokana na lalamiko hilo wanachama hao walitaka mifuko hiyo ilipie riba fedha za mafao zinazochelewa kulipwa kwa wahusika sawasawa na waajiri wanapochelewa kuwasilisha michango ya wanachama katika mifuko hiyo.
Malalamiko mengine yaliyotolewa na watumishi hao ni pamoja na uwepo wa taarifa kwamba baadhi ya mifuko hiyo haitaki kulipa mafao ya kabla ya mwaka 1999 na inataka mzigo huo ubebwe na serikali.
Mengine yanahusu baadhi ya mifuko hiyo kushindwa kuweka kumbukumbu zake vizuri pamoja na uwepo wa miongozi ya SSRA jambo linalowafanya baadhi ya wanachama wake wawe na akaunti zaidi ya moja na wakati huo huo taarifa za baadhi ya michango yao kutoonekana.
Huduma ya bima ya afya ni eneo lingine lilitajwa na wanachama hao kuwa na  changamoto kubwa kwani mbali na wanachama wake kuchangia michango yao lakini baadhi yao wameendelea kupata huduma hafifu.
Lingine linalolalamikiwa katika mifuko hiyo ni mikopo ya nyumba ambayo kwa maelezo ya wanachama ni mzigo mkubwa kwa wastaafu kwani zinauzwa zikiwa na riba wakati zimejengwa kwa fedha za wanachama.
Katika kukabiliana na changamoto za mifuko hiyo, Kasuri aliwaambia watumishi hao kwamba SSRA inaendelea kutoa elimu kwa wadau wake, inarejea miundo na kanuni zinazogongana katika sekta ya hifadhi ya jamii, inafanya tathmini za mifuko yote ya hifadhi ya jamii na inatoa miongozo ya uwekezaji.
Alisema mamlaka yao ina wajibu pia wa kupitia vikokotoo vya mafao na mafao yanayotolewa, kutathimini afya ya mifuko yote na kushauri ipasavyo, na imeielekeza mifuko yote ya hifadhi ya jamii kufanya mikutano ya wanachama.
Kwa kutambua umuhimu wa hifadhi ya jamiii kwa kila mwananchi, Kasuri alisema sheria iliyounda SSRA imeruhusu uandikishaji wa wanachama kutoka katika sekta isiyo rasmi jambo linalowanufaisha pia wakulima na wafanyabiashara wadogo.
Alisema mpaka sasa Tanzania Bara ina mifuko sita ya hifadhi ya jamii ambayo ni Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Pensheni wa PPF, Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa Serikali (GEPF), Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF), Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya (NHIF) huku Zanzibar ikiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF).
Katika kikao hicho ni mifuko miwili ya GEPF na mfuko mpya wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ilipata fursa ya kueleza majukumu yao.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...