Thursday, November 26, 2015

ZOEZI LA USAFI WA MAZINGIRA KUWA ENDELEVU JIJINI DAR ES SALAAM

index
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Mhe. Said Meck Sadiki akizungumza na waandishi wa habari ( hawapo pichani) ofisini kwake  leo  alipokuwa akizungumzia zoezi la usafi na namna mkoa ulivyojipanga kutekeleza zoezi hilo siku ya 9 Disemba.
indexx
Waandishi wa habari wakifuatilia kwa makini maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam juu ya usafi wa mazingira siku ya 9 Disemba.
indexxx
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Raymond Mushi (Kulia) akimsikiliza Mkuu wa  Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Said Meck Sadiki (Kushoto) alipokuwa akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu utekelezaji  wa  agizo la Mhe Rais la kufanya usafi wa mazingira katika maadhimisho ya sherehe za uhuru wa Tanzania Bara.                                
(Picha zote na Raymond Mushumbusi – Maelezo )
…………………………………………………………………………………………………………….
Na Lilian Lundo-MAELEZO
Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Mhe. Said Meck Sadiki amesema zoezi la usafi wa mazingira litakalofanyika siku ya Maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 9 Desemba, litakuwa ni endelevu kwa mkoa wa Dar es Salaam hata baada ya kumalizika kwa maadhimisho hayo.
 
Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Tano. Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli aliagiza kuwa Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Tanzania Bara mwaka huu yatumike kwa kufanya usafi wa Mazingira kote nchini badala ya kufanya sherehe za gwaride la askari wa vikosi vya Ulinzi na Usalama.
 
Akiongea na vyombo vya habari leo Mhe. Sadiki alianza kwa kumpongeza Mhe. Rais kwa uamuzi aliouchukua wa kubadilisha sherehe za uhuru kuwa ni siku ya kufanya kazi badala ya kwenda uwanjani na kuangalia gwaride na halaiki mbalimbali kama ilivyokuwa ikifanyika miaka iliyopita.
 
“Mhe. Rais katurejesha kule tulipotoka ambako kauli mbiu ya sherehe za uhuru ilikuwa ni uhuru na kazi au uhuru ni kazi wakati watanzania walikuwa wakiungana na kufanya kazi kwa umoja na kushirikiana,” alisema, Mhe. Sadiki.
 
Aidha, Mhe Sadiki alisema, zoezi la usafi kwa  mkoa wa Dar es Salaam litaanza rasmi tarehe  1 Disemba mwaka huu na kumalizikia 9 Disemba mwaka huu  siku ya kilele cha  maadhimisho ya siku ya uhuru na kuongeza kuwa  zoezi hilo litakuwa  endelevu.
 
Mhe. Sadiki aliongeza kwa kusema kuwa, uongozi wa mkoa umewaomba wadau kujitokeza kwa kuchangia fedha au vifaa kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo na amewataka watendaji kushawishi wananchi wa maeneo yao kutafuta vifaa badala ya kusubiri kuletewa na Halmashauri.
 
Pia, Mhe Sadiki amewahimiza watendaji wa mitaa na kata kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha maeneo wanayoyasimamia yanakuwa katika hali ya usafi muda wote ili kuepukana na magonjwa ya mlipuko na pale  inakapobainika eneo fulani lipo katika mazingira ya uchafu  basi mtendaji wa eneo hilo atawajibishwa kwa kufikishwa katika vyombo vya sheria kwa kosa la kutotimiza wajibu wake.
 
Vilevile ametoa wito kwa wananchi kuzingatia usafi  kwa kuacha tabia za kutupa taka ovyo hasa wanapokuwa katika vyombo vya usafiri na kutokujisaidia katika mitaro au vichaka ili  kuepukana na uchafuzi wa mazingira kunakopelekea kutokea kwa magonjwa ya mlipuko .

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...