Wednesday, November 25, 2015

TAMKO LA JUKWAA HURU LA WAZALENDO KUUNGA MKONO HOTUBA YA MAGUFULI

 Mwenyekiti wa Jukwaa Huru la Wazalendo Ndugu Salum Ally Hapi akizungumza na waandishi wa habari kwenye hotel ya Travetine ,Magomeni jijini Dar es Salaam, kulia ni Katibu wa Jukwaa hilo Ndugu Mtela Mwampamba.

Ndugu wanahabari,
 
 Mbele yenu sisi tuliowaita hapa ni Jukwaa Huru la Wazalendo ambalo limeitisha mkutano huu ili kufikisha yale tuliyoyakusudia kuwaeleza umma wa watanzania.

 Sote tunatambua kuwa nchi yetu imetoka katika uchaguzi mkuu ambao umetupatia viongozi wapya wa awamu ya tano ya uongozi wa taifa letu chini ya Dr. John Pombe Joseph Magufuli. Tunapenda kuwapongeza watanzania wote kwa uchaguzi wa amani na utulivu. Aidha kwakua ndio mara yetu ya kwanza kuzungumza nanyi tunapenda kuwapongeza wanahabari wote kwa kazi nzuri ambayo mmekua mkiifanya kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu nchini. Tunawashukuru sana.

 Mkutano wetu huu umebeba madhumuni makubwa mawili.
 
 Kwanza ni kumpongeza Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa  hotuba yake aliyoitoa Bungeni siku ya ufunguzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 19/11/2015. 

Tunaiunga mkono Hotuba yake ambayo kwa kweli ilikuwa imebeba Uzalendo, Ujasiri, dira ya kweli ya maendeleo ya taifa letu na muuelekeo mpya wa Serikali ya awamu ya tano. Mambo yote aliyozungumzia Mh. Rais yamebeba maslahi mapana ya nchi yetu na yanalenga kuijenga Tanzania mpya ambayo waasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume walikusudia kuijenga.

 Pili, pamoja na mambo mengi yaliyogusiwa na hotuba ya Mh. Rais, eneo la kubana matumizi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kwa Serikali ni  moja katika mambo ambayo Jukwaa hili limeamua kuyaunga mkono kwa vitendo. Mh. Rais alitoa mchanganuo wa eneo moja tu la safari za nje na jinsi lilivyo ligharimu Taifa mabilioni ya shilingi na kuahidi kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wake itajikita katika kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

 Aidha Mh. Rais ameanza kutekeleza kwa vitendo ahadi yake hiyo ya kupunguza matumizi yote yasiyo ya lazima Serikalini, ikiwemo hafla, warsha, makongamano na safari za nje. 

 Jukwaa Huru la Wazalendo, linatambua kuwa kwa miaka kadhaa mbunge wa Kigoma Mjini Mh. Zitto Kabwe amekuwa na msimamo wa kutokupokea posho za kitako tangu akiwa mbunge wa Kigoma Kaskazini katika Bunge la 10. Pamoja na mh. Zitto, Jukwaa pia limepokea taarifa za baadhi ya wabunge wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walioamua kuunga mkono juhudi za Mh. Rais za kupunguza matumizi yasiyo ya lazima serikalini kwa kukataa hadharani kupokea posho ya kitako ya mbunge (sitting allowance).

 Mnamo tarehe 23/11/2015, mbunge wa Singida Magharibi (CCM) Mh. Elibariki Imanuel Kingu alimwandikia barua Katibu wa Bunge akieleza msimamo wake wa kukataa kulipwa posho ya kitako ya Bunge (sitting allowance) katika kipindi chote cha miaka mitano (2015 -  2020). Huyu anakuwa ni mbunge wa pili baada ya Mh. Zitto Kabwe kutoka hadharani na kukataa posho ambazo msingi wake ni unyonyaji wa wanyonge na ubadhirifu wa kodi za wananchi. 

 Jukwaa linapenda kumpongeza Mh. Kingu Mbunge kwa ujasiri wake na Uzalendo kwa Taifa lake, uliomfanya kuunga mkono juhudi za Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa vitendo. 

 Jukwaa linatambua ya kwamba, mapambano ambayo Mh. Kingu Mbunge ameyaanzisha ni makubwa, magumu na yanahitaji kuungwa mkono na watanzania wote wanaoipenda nchi yao bila kujali itikadi za vyama. Tunafahamu, wapo baadhi ya wabunge wabinafsi na wasio na huruma na wanyonge wa Taifa letu ambao hawajafurahishwa na hatua hii ya wabunge kama Zitto na Kingu ya kukataa posho ya kitako. Baadhi ya wabunge wameanza kumpigia simu na kumtumia jumbe (sms) za vitisho mh. Elibariki Kingu (MB) na wengine wakibeza kuwa anatafuta cheo.

 Jukwaa linalaani hatua za wabunge hao wanaopinga nia njema ya Mh. Elibariki Kingu na Mh. Zitto Kabwe kwa uamuzi wao wa kukataa posho za kinyonyaji na hivyo basi, Jukwaa linawaomba wananchi wote majimboni, kuwataka wabunge wao waliowachagua kueleza misimamo yao hadharani juu ya kuunga mkono hatua ya kukataa posho kama njia ya kupunguza matumizi ya Serikali yasiyo ya lazima.

 Jukwaa linafahamu ya kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya kuidhinisha masharti ya kazi za kibunge na stahiki wanazopaswa kulipwa katika kazi hiyo.Kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, tunamuomba na kumshauri Mh. Rais John Pombe Magufuli atakapokuwa anaidhinisha masharti na stahiki hizo, atusaidie kuifuta kabisa posho ya kitako ya wabunge (sitting allowance). 

 Aidha, Jukwaa linamuomba mh. Rais kuzipitia na kutoa agizo la kufutwa kwa posho zote zisizo za lazima zinazolipwa kwa watumishi wa umma wa kada mbalimbali yakiwemo mashirika ya umma.
 
 Jukwaa letu linatoa wito kwa wabunge wote bila kujali vyama vyao, kuungana na Mh. Kingu(MB) na Mh. Zitto(MB) katika kukataa malipo ya posho ya kitako ili kupunguza mzigo mkubwa ambao Serikali inaubeba kuhudumia wabunge. Fedha hizi ni vyema zielekezwe katika kutatua kero za wananchi vijijini kama vile ukosefu wa maji, madawati, vitanda vya Hospitali n.k.

Tunasisitiza kwamba, Ubunge ni Utumishi,na wala sio Utukufu. Kazi ya Mbunge ni kuwawakilisha wananchi wake na si kuwanyonya. Tufike mahali kama Taifa tuwe na nidhamu ya matumizi ya kodi za wananchi na mgawanyo sawa wa keki ya Taifa. Kuendelea kulipana posho hizo ni ishara ya unyonyaji, dhuluma na kuongeza pengo kati ya wenye nacho na wasionacho nchini. Jambo hili linakuza chuki na hasira miongoni mwa wananchi wa hali ya kawaida dhidi ya viongozi wao na serikali kwa ujumla.

 Tunawaahidi kuwa Jukwaa litaendeleza harakati (movement) na vuguvugu hili kwa kuanzia na Bunge kwasababu ndio wawakilishi wa wananchi. Tutaendelea kupaza sauti zetu ili wabunge wengi zaidi Wazalendo wajitokeze na kukataaa posho hizi. Tunajua kuwa wapo miongoni mwao wabunge wazalendo ambao wataguswa na wito huu na kuuunga mkono hadharani. 

 Aidha tutaendelea kuwasemea kwa wananchi wabunge ambao bado hawataki kukataa posho hizi bila kujali vyama vyao. Tunawaomba wananchi kote nchini kutuunga mkono katika harakati hizi ili tuweze kuokoa mabilioni ya shilingi yanayopotea kila Bunge linapokaa Dodoma kupitia posho ya kitako (sitting allowance).

Tutaandaa maandamano nchi nzima ya kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kuwashinikiza wabunge kukataa posho hizi. Makongamano na mdahalo mbalimbali itaandaliwa na jukwaa ili kujenga uelewa wa pamoja wa wananchi na kuwa na sauti moja katika kupinga posho za wabunge, watumishi wa serikali na mashirika ya umma. Haya yatafanyika katika kufikia kusudio letu la kumuunga mkono Mheshimiwa Rais katika hatua yake ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kwa Serikali. 


Hatutaogopa wala kutishwa na yeyote katika kutekeleza jukumu hili zito. 


 Ahsanteni sana.

 ALLY SALUM HAPI  - MWENYEKITI
 MTELA MWAMPAMBA  - KATIBU

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...