Afisa michezo mkoa wa Mwanza, James William, akimkabidhi zawadi ya kitita cha shilingi milioni moja na nusu mshindi wa kwanza wa mbio za km 21 upande wa wanawake Alice Mogire kutoka Kenya baada ya kutumia muda wa saa 01:14:42 kumaliza mbio hizo. Wanaoshuhudia ni Meneja Mkuu kampuni ya Capital Plus International Limited ambao ni waandaaji wa mashindano hayo, Erasto Kilawe (kushoto), Meneja Kiongozi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) mkoa wa Mwanza, Hamis Faki (wa pili kushoto), mjumbe wa shirikisho la riadha Tanzania (RT), Peter Mwita (wa pili kulia) na Mwenyekiti wa chama cha riadha mkoa wa Mwanza, Silas Lucas.
Washindi wa nafasi tatu za juu katika mbio za km 21 upande wa wanaume wakionyesha medali na pesa taslimu walizopokea kama zawadi baada ya kuibuka washindi katika mbio hizo.
Mwenyekiti wa chama cha riadha mkoa wa Mwanza Silas Lucas akiwapa maelekezo wakimbiaji wa km 21 wakati wa mbio za Rock City Marathon kabla ya mbio kuanza kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza jana.
Wanariadha katika kundi la km 21 wakikatiza katika mitaa ya jiji la Mwanza kuelekea katika viwanja vya CCM Kirumba kumaliza mbio hizo.
Festus Taram kutoka Kenya akimaliza katika nafasi ya kwanza kwenye mbio za Rock City Marathon zilizofanyika jijini Mwanza jana baada ya kutumia muda wa saa 01:04:40, akifuatiwa kwa karibu na mshiriki mwenzake kutoka nchini humo Evancy Kiplagan aliyetumia muda wa saa 01:04:55
Raia wa kigeni nao walijitokeza kuchuana vikali katika mbio hizo.
Wanariadha wakianza kukimbia mbio za km 21 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza jana, wakati wa mbio za Rock City Marathon 2015.
Wanariadha katika kundi la kilomita tano wakipasha kabla ya kuanza kwa mbio hizo.
Mwandishi wetu, Mwanza
Festus Taram kutoka Kenya aliibuka mshindi wa kwanza kwenye mbio za Rock City Marathon zilizofanyika jijini Mwanza jana baada ya kumaliza kwa muda wa saa 01:04:40, akifuatiwa kwa karibu na mshiriki mwenzake kutoka nchini humo Evancy Kiplagan aliyetumia muda wa saa 01:04:55
Mbio hizo za kilomita 21 zilianzia Uwanja wa CCM Kirumba kupitia Barabara ya ikulu ndogo hadi mzunguko wa samaki na kuelekea Buzuruga kisha kutokea barabara ya pasiansi na kumalizikia uwanjani Kirumba.
Nafasi ya tatu upande wa wanaume ilichukuliwa na Mtanzania Fabian Joseph aliyetumia muda wa saa 01:05:00, ikiwa dakika chache nyuma ya mpinzani wake.
Akizungumzia siri ya ushindi wake, Talam alisema hii ni mara ya pili kushiriki mashindano hayo ambapo mwaka jana alishika nafasi ya tatu jambo lililompa chachu ya kujituma kufanya mazoezi zaidi na kukaa kambini muda mrefu jambo lililopelekea kufanya vizuri katika michuano ya mwaka huu.
“Maandalizi ya mwaka huu ni mazuri na washiriki wameendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka jambo linalotufanya wanariadha kujiwekea mikakati mizuri ili kuweza kukabiliana na ushindani mkali uliopo katika mbio hizi,” alisema.
Upande wa wanawake mshindi wa kwanza ni Mkenya Alice Mogire aliyetumia muda wa saa 01:14:42 akifuatiwa na Mtanzania Natalia Elisante aliyetumia saa 01:15:16 huku Raia mwingine wa Tanzania Angelina Isere akishika nafasi ya tatu baada ya kutumia saa 01:15:35
Washindi wa kwanza katika mbio hizo zilizofanyika kwa mara ya saba jijini Mwanza waliibuka na kitita cha Sh1.5 milioni kila mmoja, washindi wa pili Sh900,000 na washindi wa tatu Sh700,000 kila mmoja.
Mashindano hayo ya kila mwaka yaliyo katika kalenda ya RT yaliandaliwa na Kampuni ya Capital Plus kwa udhamini wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bank M, Precision Air, New Mwanza Hotel, Bodi ya Utalii Tanzania na PPF.
Wakati huohuo, Katibu tawala mkoa wa Mwanza alipongeza waandaaji wa mbio hizo na kutoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana kwa pamoja ili kurejesha hadhi ya mchezo wa riadha nchini.
Akikabidhi zawadi kwa washindi wa mbio hizo kwenye uwanja wa CCM Kirumba kwa niaba ya Katibu tawala jana, Afisa michezo mkoa wa Mwanza, James William, alisema mbio hizo ni nyenzo muhimu ya kuwaandaa wanariadha wetu nchini kuwa katika nafasi ya kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa na kuirudishia nchi yetu heshima ya kipekee katika mchezo huo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
No comments:
Post a Comment