Thursday, November 19, 2015

BALOZI WA UINGEREZA NCHINI AONGOZA UZINDUZI WA FILAMU YA KUPINGA UKEKETAJI YA SIMULIZI HALISI YA GHATI NA RHOBI

 Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Dianna Melrose (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Wanawake wa Afya, Utafiti na Maendeleo (Forward), Naana Otoo-Oyortey MBE, wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa Filamu ya Simulizi halisi ya Ghati na Rhobi ulifanyika nyumbani kwa balozi huyo, Oysterbay Dar es Salaam jana.
 Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Dianna Melrose (kulia), akizungumza kabla ya uzinduzi wa filamu hiyo.
 Mwakilishi kutoka taasisi ya DFID, Jane Miller OBE (kushoto), akizungumza katika uzinduzi huo. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Wanawake wa Afya, Utafiti na Maendeleo (Forward), Naana Otoo-Oyortey MBE.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Wanawake Tanzania, Mary Rusimbi (kulia), akizungumza katika uzinduzi huo.
 Wadau mbalimbali wakiwa kwenye uzinduzi huo.
 Sehemu ya filamu hiyo inavyoonekana.
 Sehemu ya filamu hiyo inavyoonekana.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Wanawake wa Afya, Utafiti na Maendeleo (Forward), Naana Otoo-Oyortey MBE (katikati), akichangia jambo katika uzinduzi huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti (kulia), akielezea kuhusu filamu hiyo na changamoto mbalimbali za ukeketaji nchini.
……………………………………………………………………………………
Na Dotto Mwaibale
 
LICHA ya MKOA wa Dar es Salaam kuwa na watu wenye uelewa mkubwa lakini unaongoza kwa asilimia 38 ya ukeketaji imeelezwa.
 
Hayo yalibanishwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto Wizara ya Wanawake na Watoto, Margaret Mussai Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa Filamu ya Simulizi halisi ya Ghati na Rhobi uliofanyika nyumbani kwa Balozi wa Uingereza hapa nchini.
 
“Hali ya ukeketaji hapa nchini bado ni changamoto kubwa kutokana na jamii kutokuwa na uelewa mkubwa ikiwa ni pamoja na mila za baadhi ya makabila” alisema Mussai.
 
Alisema suala la ukeketaji limekuwa na changamoto kubwa kwa sababu ya wahusika wanaofanya ukeketaji wanatengeneza fedha na kwa msichana anayefanyiwa kitendo hicho anaonekana kuwa na thamani kuliko yule ambaye hajakeketwa.
 
Alisema kwa mkoa wa Dar es Salaam kuna maeneo ambayo yanaongoza kwa ukeketaji na wasichana hupenda kufanyiwa hivyo ili waonekane wenye heshima.
 
Alisema mkoa wa Dar es Salaam una asilimia 38 ya ukeketaji, Mara asilimia 58, Shinyanga asilimia 55 huku ikifuatia mikoa mingine.
 
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Dianna Melrose filamu hiyo inawahusu wasichana wawili ambao wanapinga ukeketaji katika jamii yao.
 
Alisema wasichana hao waqnaonesha ujasiri wa kukataa kitendo hicho chenye maumivu makali na kwa msaada wanafanikiwa kubadisha jinsi jamii yao inavyomchukulia msichana katika kipindi chake cha mpito kutoka usichana hadi kwenda kufikia utu uzima.
 
“Filamu hii inaonesha kwamba si jamii zote ndani ya Tanzania zinazojihusisha na ukeketaji na kwamba maeneo mengi wameamua kuachana na ukeketaji na kuamini kwamba ukeketaji unawezwa kutokomezwa” alisema Melrose.
 
Alisema mtoto wa kike ana haki ya kusomeshwa na kuendelezwa badala ya kuachwa nyumbani na kufanyiwa vitendo hivyo vinavyodumaza jamii kimaendeleo.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti alisema changamoto kubwa ni sheria ya makosa ya ukeketaji kuto kuwa na meno kwani ni mtu mmoja tu aliyehukumiwa kati ya watu 43 waliobainika na makosa hayo.  
  
Filamu hiyo imeandaliwa na ubalozi huo kwa kushirikiana na Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) na Mfuko wa Wanawake wa Afya, Utafiti na Maendeleo (Forward).

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...