Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ambaye ni mlezi wa Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (TADWU), akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam nje ya chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Taifa ya kuhusu kifo cha utata cha aliyekuwa Katibu wa chama hicho Tanzania, Rashid Saleh kilichotokea hivi karibuni pamoja na ratiba ya mazishi yake yatakayofanyika jijini Mwanza.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ambaye ni mlezi wa Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (TADU), akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Global Pubrishers LTD, Eric Shigongo (katikati), na wadau wengine kuhusu taratibu za mazishi za katibu huyo.
Mjumbe wa Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (TADWU), Stanley Kilave (kulia), akizungumza na Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Clement Masanja (kushoto), pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Global Pubrishers LTD, Eric Shigongo (katikati), wakati wa taratibu za mazishi zikifanyika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dar es Salaam.
Msemaji wa familia ya marehemu, Jonas Marinyizu (katikati), akitoa shukurani kwa DC Makonda na wadau wengine kwa kuwezesha msiba huo pamoja na utaratibu wa mazishi utakavyo kuwa.
Mwenyekiti wa Chama hicho, Shaban Mdem akizungumza katika mkutano na wanahabari
Ndugu na jamaa wa marehu wakiwa katika chumba za kuhifadhi maiti Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakisubiri kufanyika taratibu cha uchunguzi wa mwili huo kabla ya kusafirishwa kwenda jijini Mwanza kwa mazishi.
Ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu wakiwa katika chumba za kuhifadhi maiti Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakisubiri kufanyika taratibu cha uchunguzi wa mwili huo kabla ya kusafirishwa kwenda jijini Mwanza kwa mazishi.
…………………………………………………………………………………………………
…………………………………………………………………………………………………
Na Dotto Mwaibale
MWILI wa Katibu Mkuu na Msemaji wa Chama Cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (TADWU), Rashid Saleh umesafirishwa jana kwenda kijijini kwao Kayenze wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza kwa maziko.
Saleh alifariki Ijumaa Novemba 20 Majira ya saa 8 mchana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wakati akipata matibabu ya maradhi ya figo ili kuokoa maisha yake baada ya kile kinachodaiwa kushindwa kufanya kazi ipasavyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ambaye pia ni mlezi wa chama hicho, Paul Makonda alisema kuwa wamepata pigo kutokana na umuhimu na umahiri ambao alikuwa nao marehemu hasa katika kutetea haki za madereva wenzake sanjari na kuibua mambo mbalimbali ambayo yatabaki kuwa historia na kumbukumbu kwao.
“Saleh alifariki jana (Novemba 20) baada ya kusikia anaumwa ambapo hali yake haikuwa nzuri na madaktari walishauri nimlete Muhimbili kwa matibabu zaidi ambapo nilimfikisha lakini baada ya muda mfupi wakati madaktari wanahangaika kumtibu na kuokoa maisha yake alifariki,”alisema.
Alisema marehemu amekiacha chama sehemu ya mafanikio makubwa zaidi ya mabadiliko na mikataba ya haki za madereva nchi nzima huku akibainisha mazingira ya kifo na kutaka uchunguzi zaidi ili kujiridhisha na kifo chake uliofanywa chini ya uangalizi wa polisi.
“Hatukuona kama kuna haja ya kumuhifadhi mwili wa ndugu yetu hadi hapo tutakapojua nini chanzo cha kifo chake kwani majibu ndiyo yatatupa picha ya ugonjwa kwani tumehangaika tangu alipokuwa hospitali ya Kairuki ambapo tulipofika hapa ikabainika kuwa figo zake zote mbili hazifanyi kazi,”alisema.
Aliongeza kuwa marehemu alipelekwa hospitalini hapo kwa kitengo maalum huku akibainisha endapo figo zinashindwa kufanya kazi mzunguko mzima wa damu mwilini nao husimama ambapo madaktari walishirikiana lakini hawakuweza kuokoa maisha yake.
Mwenyekiti wa Chama hicho, Shaban Mdem alisema kuwa msiba huo umewasikitisha sana kutokana na mazingira ya kifo chake huku akiitaka mamlaka husika kulisimamia suala hilo la kupatika kwa majibu sahihi juu ya kifo chake.
“Tunataka uchunguzi ufanyike na majibu yatoke yakiwa sahihi na yanayoridhisha juu ya kifo chake kwani amekufa na madai ambayo yapo ndani yao, hivyo serikali itambue kifo cha Saleh ni katika harakati za kudai haki ambayo tuliyawasilisha mbele ya aliyekuwa waziri mkuu Mizengo Pinda,”alisema.
Alisema Saleh ni kiongozi wa taifa zima hivyo alimtaka rais Magufuli kuingilia kati suala hilo kwani kutokana na hali hiyo watamaliza wafanyakazi wote kwa kuwauwa katika mazingira kama hayo sambamba na kutenga siku rasmi kwa ajili ya maombezo ya msemaji huyo.
Mazingira ya Kifo
Akizungumzia mazingira ya kifo Msemaji wa Familia ya Marehemu Jonas Ernest alisema kuwa Novemba 9 mwaka huu marehemu alipokea simu kutoka kwa rafiki yake ma kumtaka waende kwenye kikao, ambapo baada ya hapo mwenzake alidai kuwa na njaa.
Alidai baada ya hapo walikwenda kuagiza chakula ambapo mwenzake hakula na kumuacha marehemu akiwa anakula huku mwenzake akiwa amemuaga kwenda msalani.”Baada ya kurudi msalani alimkuta marehemu akilalamika tumbo linamuuma na hivyo kuondoka eneo hilo pasi na huyo rafiki kula chochote,”alisema.
Alidai kuwa baada ya kuhisi maumivu makali ya tumbo alianza kuharisha na kutapika na alikimbizwa hospitali lakini uchunguzi ulibaini hakuwa na tatizo na kurudishwa nyumbani ambapo siku inayofuata alirudi hospitali na kuambiwa kuwa ana malaria 4.
“Alianza kutumia dawa za malaria na baadaye kujiskia vibaya na kumrudisha tena hospitali ya Kairuki laikini madaktari walidai kuwa anatatizo ndani ya mwili ambalo ni figo kushindwa kufanya kazi vizuri,”alidai na kuongeza kuwa hadi marehemu anafariki alikaririwa akidai kuwa”Nyama inanitenganisha na mwanangu lakini”na kumtaja mmoja wa wafanyakazi wenzake huku akidai kumuona mtoto wake.
Harakati za kudai haki ya madereva
Saleh alizaliwa mwaka 1966 Mwanza, ambapo hadi anafariki alikuwa katika harakati za kudai na kutetea haki za madereva ambapo Oktoba 2, mwaka huu alikaririwa akisema wamechoshwa na uozo unaoendelea kufanywa na Mamlaka ya Usafirishaji Majini na Nchi Kavu (Sumatra) na Wizara ya Kazi na Ajira kuhusu kufumbia macho kero zinazoitatiza sekta ya usafirishaji hasa kwa madereva wa mabasi ya abiria na magari ya mizigo.
No comments:
Post a Comment